Mbunge wa Mtwara Vijijini Mhe. Hawa Ghasia ameonesha uwezo mkubwa wa kuogelea wakati wa tamasha la “Msangamkuu Beach Festival “lililofanyika Disemba 30,2018.
Ghasia ambaye anadai ana uzoefu wa kuogelea maji ya bahari tangu akiwa mtoto aliuacha hoi umati huo kwa jinsi alivyokuwa akibadili mitindo mbalimbali ya kuogelea hali ambayo ilizifanya meli za uokoaji kumzunguka mara kwa mara ili kujiridhsiha iwapo hayuko matatizoni.
Akizungumzia tamasha hilo Mhe. Ghasia amepongeza hatua hiyo na kuwataka wanachi na wawekezaji wa nje na ndani ya mkoa kujitokeza kwa wingi kuwekeza katika wilaya ya Mtwara, ambayo ina fukwe nyingi za kuvutia.
Amezitaja fukwe hizo kuwa ni pamoja na Msimbati ambayo ameitaja kama fukwe pekee hapa nchini ambayo binadamu anaweza kuendesha gari kama anavyoendesha kwenye barabara ya lami, fukwe ya Mnazi ambayo ina urefu zaidi ya kilometa ishirini, fukwe ya Naumbu pamoja na ile ya Mgao.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Evod Mmanda amewapongeza wanaMtwara waliojitokeza katika tamasha hilo. Anasema Msangamkuu ni eneo moja katika maeneo mengi yanayohitaji kutangazwa hivyo atahakikisha dunia inatambua hilo.
Tamasha la “MsangaMkuu Beach festival” limefanyika kwa mara ya kwanza katika fukwe hiyo Disemba 30,2018 huku mwanzilishi wa tamasha hilo Mhe. Gelasius Byakanwa, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara akiwaomba wadhamini kujitokeza kudhamini tamasha hilo ambalo anakusudia liwe endelevu. Amesema hiyo ni fursa muhimu kwa kutangaza vivutio vya utalii vya mkoa wa Mtwara.
Video yake hii HAPA
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.