Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Glasius Gasper Byakanwa (Kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Evod mmanda mara baada ya kuwasili kwa mara ya kwanza katika Ofisi yake jana.
Mtwara itajengwa kwa ushirikiano -RC Byakanwa
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Gasper Byakanwa amewataka wananchi wa Mkoa wa Mtwara kutoa ushirikiano ili kufikia malengo katika kusukuma maendeleo ya mkoa. Amesema njia pekee ya kuweza kufikia malengo ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa Mkoa wa Mtwara ni ushirikiano kati ya viongozi na wananchi kwa ujumla. Hayo ameyasema leo mara baada ya kukabidhiwa ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo Mheshimiwa Halima Dendego.
Mheshimiwa Byakanwa ambaye amehamishwa kutoka nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Hai amezitaja baadhi ya changamoto za mkoa wa Mtwara kuwa ni pamoja na elimu. Amesema haridhishwi na matokeo ya mitihani ya kitaifa kwa mkoa wa mtwara ukiwemo mtihani wa darasa la saba mwaka 2017 ambapo Mkoa wa Mtwara umeingia katika nafasi kumi za mwisho kitaifa
‘Mimi siku zote huwa napenda kuwa wa kwanza hivyo sikubali kushikilia nafasi za mwisho katika nafasi yoyote’. Amesema Byakanwa
Kuhusu kuinua zao la korosho ambalo ni moja ya mhimili wa uchumi wa mkoa wa Mtwara amesema ni moja ya vipaumbele vyake. Anasema korosho ni dhahabu ya kijani kwa wananchi wa Mkoa wa Mtwara, hivyo lazima ahakikishe inamkomboa Mkulima wa Mtwara.
Kwa upande wake aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Halima Dendego amesema anashukuru kwa hatua iliyofikiwa katika maendeleo ya mkoa wa Mtwara. pia amemshukuru Mheshimiwa Rais aliyemuamini kwa kipindi chote ambacho amekuwepo Mkoani Mtwara. amesema anauacha Mkoa wa Mtwara ukiwa salama pia ukijitosheleza kwa chakula. Amewaomba wanamtwara kutoa ushirikiano kwa Mheshimiwa Byakanwa ili Mtwara ing’ae zaidi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.