1. UTANGULIZI
1.1 TASWIRA YA HALMASHAURI YA WILAYA YA NANYUMBU
Halmashauri ya wilaya ya Nanyumbu, ni moja kati ya Halmashauri tisa za mkoa wa Mtwara. Halmashauri hii ilianzishwa chini ya Sheria namba 7 ya mwaka 1982 ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) na kutangazwa rasmi katika Gazeti la Serikali Na. 190 la tarehe 01 Julai 2007. Makao makuu ya Wilaya yapo mji wa Mangaka ambao upo umbali wa kilomita 54 kutoka Masasi kwenye barabara ya Mtwara-Songea.
Asili ya wenyeji wa wilaya ya Nanyumbu ni makabila ya wamakua, wayao, na wamatambwe ambao huzungumza lugha zao za asili pamoja na Kiswahili.
1.2 MIPAKA YA ENEO
Wilaya hii iko kati ya latitudo 360 na 380 mashariki mwa Greenwich na latitudo 100 na 120 kusini mwa Ikweta. Nanyumbu inapakana na wilaya ya Nachingwea upande wa kaskazini, wilaya ya Masasi kwa upande wa mashariki, wilaya ya Tunduru upande wa magharibi na Jamhuri ya Msumbiji kwa upande wa kusini.
1.3 HALI YA HEWA
Hali ya hewa katika wilaya ya Nanyumbu ni joto la wastani ambalo ni 25 0C huku joto la juu likiwa 32 0C. Kipindi cha Desemba hadi Aprili, upepo unaojaa unyevunyevu kutoka Kaskazini-Mashariki huelekea Kusini Magharibi na kupelekea msimu wa mvua wenye joto na unyevunyevu. Aidha, kipindi cha Mei hadi Novemba, upepo kutoka Kusini Mashariki husababisha wilaya kuwa kavu, baridi na isiyo na unyevunyevu. Wilaya hupata mvua ya wastani wa 832 mm ambayo hunyesha msimu mmoja kwa mwaka kuanzia mwezi Desemba hadi Aprili.
1.4 ENEO LA KIUTAWALA
Wilaya ya Nanyumbu ina tarafa nne za kiutawala ambazo ni Nakopi, Nanyumbu, Mangaka na Maratani pamoja na jimbo moja la uchaguzi (Jimbo la Nanyumbu). Wilaya imegawanywa katika kata 17, vijiji 93 vilivyosajiliwa na vijiji vidogo 526. Wilaya ya Nanyumbu ni kubwa kijiografia ikilinganishwa na halmashauri zingine za mkoa wa Mtwara kwani ina eneo la ukubwa wa kilomita za mraba 5,071.5. Ukubwa wake wa kijiografia ni asilimia 30 ya Mkoa mzima ambao una eneo la ardhi la kilomita za mraba 16,720.
Ugawaji wa eneo la ardhi katika wilaya ya Nanyumbu unaonesha kuwa, tarafa ya Nakopi inachukua sehemu kubwa ya eneo la ardhi ikiwa na kilomita za mraba 1665.7, ikifuatiwa na tarafa ya Nanyumbu yenye kilomita za mraba 1628. Tarafa ya Mangaka ina kilomita za mraba 1040.4 huku tarafa ya Maratani ina eneo la jumla ya kilomita 737.4 za mraba.
1.5 IDADI YA WATU
Kwa Mjibu wa Sensa ya Kitaifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Wilaya ilikuwa na Jumla ya wakazi wapatao 204,323 ambao ni wanawake 104,625 na wanaume 99,698.
1.6 SHUGHULI ZA KIUCHUMI
Zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wa Wilaya ya Nanyumbu hujishughulisha na shughuli za kilimo kwa ajili ya chakula na biashara. Mazao ya biashara yanayolimwa ni korosho, ufuta, karanga, choroko na mbaazi. Mazao ya chakula ni mahindi, mpunga, muhogo, mtama, mbaazi, njugumawe, kunde na upupu. Aidha, baadhi ya wakazi hujishughulisha na uvuvi katika mto Ruvuma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.