Mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Newala kufatilia vikundi ambavyo vilipata mikopo ya asilimia Kumi na havijarejesha mikopo yao kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo.
Kanali Sawala amesema hayo kwenye baraza maalum la madiwani lililokuwa linajadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Kanali Sawala ameongeza kuwa Halmashauri hiyo ilikopesha vikundi shilingi milioni Themanini na Tano lakini ni vikundi vichache ambavyo vimeweza kurejesha fedha.
Aidha ametumia baraza hilo kuwataka viongozi wa Halmashauri hiyo kuendelea kujipanga ili kuongeza mapato ya Halmashauri.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Newala Mwangi Kundya amesema Halmashauri hiyo imeendelea kufanya vizuri katika makusanyo yake na wanaendelea kubuni vyanzo mbalimbali vya mapato ili kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo.
Akihitimisha kikao hicho cha baraza maalum la madiwani mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ameipongeza serikali kwa kuendelea kuleta fedha za kujenga miradi ya maendeleo ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Halmashauri ya wilaya ya Newala imepata hati safi kwa mwaka wa fedha 2022/2023 huku Mkuu wa Mkoa akiwataka viongozi wa Halmashauri hiyo na wataalam kuhakikisha wanajibu hoja moja iliyobaki na taarifa ya utekelezaji wa hoja hiyo ufike ofisini kwake.
Juni 27, 2024.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.