Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema kuwa ni vyema Halmashauri na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kushirikiana katika kuboresha utoaji wa huduma za Leseni hali ambayo itaweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wafanyabiashara wetu na hivyo kuongeza wigo wa walipa kodi.
Kanali Abbas ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya siku tatu ya Maafisa Biashara kutoka katika mikoa 10 ya Tanzania Bara, kwenye Ukumbi wa Boma mkoani Mtwara huku akiwakumbusha BRELA kuwa jukumu mojawapo la Kisheria la BRELA ni utoaji wa Leseni za Biashara kundi “A” kama ilivyo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGAs) Tanzania Bara, ambazo kwa kupitia Sheria hiyo hiyo ya Leseni za Biashara zinatoa Leseni za Biashara kundi “B”, hivyo ni muhimu kushirikiana.
“Kwakuwa Sheria ya Leseni za Biashara inasimamiwa na kutekelezwa na Mamlaka hizi mbili yaani BRELA na Halmashauri, kuna umuhimu wa Mamlaka hizi mbili kufanya kazi kwa ukaribu na kwa kuelewana na kushauriana njia bora za kuboresha utoaji wa huduma za Leseni na kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wafanyabiashara wetu na hivyo kuongeza wigo wa walipa kodi, kuongezeka kwa ajira na ukuaji wa uchumi wa nchi kwa ujumla wake”,aliongeza Mhe. Kanali Ahmed.
Akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, Mkuu wa Sehemu ya Leseni za Biashara, Bw. Tawi Kilumile ameeleza kuwa ana matarajio na elimu hiyo itakayotolewa na kwamba Maafisa Biashara hao watakuwa Mabalozi wazuri kwa maafisa wengine.
“Katika mikakati ya BRELA kutumia rasilimali za Taifa vizuri na kwa pamoja, BRELA imeona kuna umuhimu wa kufanya mafunzo haya ya kuwajengea uwezo Maafisa Biashara wa Mikoa na Halmashauri zote ili waweze kuielewa kiundani Sheria ya Leseni za Biashara (Sura 208) na Sheria ya Taifa ya Usajili na Utoaji wa Leseni za Viwanda (Sura 46).
Hivyo ni imani yangu kuwa mnakwenda kuwa mabalozi wazuri wa BRELA na Serikali kwa ujumla na kuwa mfano bora kwa Maafisa wengine katika utoaji wa huduma bora na wezeshi”, ameeleza Bw. Kilumile.
Maafisa Biashara kutoka Mikoa ya Lindi, Ruvuma, Njombe, Iringa, Songwe, Mbeya, Pwani, Morogoro, Dar es Salaam na Mtwara wamepata mafunzo ya siku tatu kuanzia Mei 10 hadi 12, 2023.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.