Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema ruzuku ya mbolea inayotelewa na Serikali imesaidia kuongeza tija kwa wakulima ambapo idadi kubwa ya wakulima wamejitokeza kuchangamkia fursa hiyo, hatua ambayo imechangia katika kumkwamua mkulima na kuchangia pato la mkoa.
Kanali Abbas ametoa kauli hiyo ofisini kwake Mjini Mtwara katika mahojiano na wataalamu kutoka Wakala wa mbolea Nchini TFRA chini ya Wizara ya Kilimo ambapo amesema uamuzi wa Serikali wa kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima ni hatua inayopaswa kuungwa mkono na kila mdau kwani kwa kiasi kikubwa umempunguzia mkulima mzigo wa gharama za uzalishaji.
Pia Mkuu wa Mkoa Kanali Abbas ameongeza kuwa kabla ya kuanza kutumia mfumo wa ruzuku mkulima alilazimika kununua kg. 50 za mbolea kwa gharamaya shilingi 140,000 lakini baada ya serikali kuanza kusambaza mbolea ya ruzuku, hivi sasa mkulima anapata kiwango kile kile cha mbolea kwa gharama ya shilingi 70,000 tu.
“Kwa dhati kabisa naishukuru serikali inayoongozwa na Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wakuinua sekta ya kilimo, ili iweze kutoa tafsiri halisi ya kuchangia kukuza uchumi na pato la taifa kwa ujumla” alisema Kanali Ahmed Abbas Ahmed.
Halikadhalika kuhusu mchango wa sekta ya kilimo katika pato la Mkoa, Kanali Abbas amesema kati ya mwaka 2021/2022 pato la Mkoa lilikuwa shillingi trilioni 3.4 lakini kutokana na maboresho yaliyofanyika katika sekta ya kilimo hivi sasa pato limepanda na kufikia shilingi trillion 4, ongezeko ambalo pia limechangiwa na uzalishaji wa mazao ya kimkakati ikiwemo korosho na ufuta.
“Sisi Mtwara tuna eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 17,620 ndani ya eneo hilo jumla ya hekta 1,672,000 ndizo zinafaa kwa kilimo, lakini sio zote zinazotumika kuzalisha” alisisitiza Mhe Kanali Ahmed Abbas Ahmed.
“Hivyo sisi tumejiwekea mikakati kama Mkoa itakayotusaidia kuongeza tija katika sekta hii, kwanza tunahakikisha tunahamasisha wakulima wetu kujisajili katika kanzi data, ambapo awali tulikadiria kusajili wakulima 77,901 lakini tumejikuta tunavuka lengo kwa kusajili wakulima 88,678. Pia tunahakikisha wataalamu wetu wa kilimo (Maafisa Ugani) wanawatembelea wakulima na kuwapa elimu” alisisitiza Kanali Ahmed Abbas Ahmed.
Aidha Kanali Abbas ameishukuru Serikali kwa kuupatia Mkoa wa Mtwara tani 1385 za mbolea ya ruzuku ambapo mpaka sasa jumla ya tani 907 ndizo zimegawiwa kwa wakulima.
Kanali Abbas ameongeza kuwa serikali ya Mkoa itawasiliana na Wizara ya Kilimo ili kuona uwezekano wa kuvitumia vyama vya msingi vya ushirika ambayo ndio viko karibu zaidi na wakulima, vishiriki katika zoezi la kugawa mbolea ya ruzuku ili kumpunguzia adha mkulima ambaye amekuwa akilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo.
“kwa vile nyinyi ndio wawakilishi wa Wizara naomba mpeleke ombi langu la kuongeza vituo vya kusambazia mbolea yaruzuku, sisi Mkoa tutawahamasisha wadau wanaohitaji kuwa mawakala wajitokeze, kuhusu suala la matumizi sahihi ya mbolea, panueni wigo wa kutoa elimu” alisisitiza Kanali Ahmed Abbas Ahmed.
Kwa upande wake kaimu meneja ukaguzi wa mbolea kutoka wakala wa mbolea nchini (TFRA) Dkt. Asheri Kalala amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa tayari Wizara ya kilimo imeandaa utaratibu mzuri utakaorahisisha upatikanaji wa mbolea katika maeneo yote nchini.
“Mhe Mkuu wa Mkoa kweli kabisa katika baadhi ya maeneo wakulima wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata mbolea lakini baada ya Wizara kubaini changamoto hiyo, tayari imeviagiza vyama vya ushirika kuwatembelea wakulima na kupata mahitaji yao na kasha kuwasiliana na Wizara ili vipate kibali cha kuwahudumia kwa ujumla hatua hii itasaidia kupunguza adha ya msongamano katika vituo halikadhalika kusafiri umbali mrefu” aliongeza Dkt. Kalala.
Kuhusu mkakati wa kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea, Dkt. Kalala amesema kuwa wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo tayari wameanza kutoa elimu hiyo katika Mikoa ya Lindi na Mtwara tangu mwaka 2021 hatua ambayo amesema imechangia kuongeza kiwango cha uzalishaji mashambani.
Kanali Ahmed Abbas Ahmed pia ameitumia fursa hiyo kuwahamasisha vijana kuchangamkia fursa ya kuingia katika sekta ya kilimo kama ambavyo serikali ya awamu ya sita imekuwa ikiwahamasisha na kuahidi kuwapatia ardhi na elimu ya kuendesha kilimo kwa tija.
Katika mwaka wa fedha 2022/2023 serikali imetumia kiasi cha shilingi Billioni 150 kwa ajili ya kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima nchi nzima huku Mkoa wa Mtwara ukiwa ni miongoni mwa Mikoa iliyonufaika.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.