CRDB wapiga Tafu mapambano ya CORONA Mtwara
Katika kuhakikisha jamii ya wanaMtwara wanakuwa salama dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 Benki ya CRDB Tawi la Mtwara imetoa msaada wa ndoo za 30 za kunawia pamoja na sabuni galoni 14. Vifaa hivyo vimekabidhiwa leo Aprili 16, 2020 kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasisus Byakanwa katika tukio fupi lililofanyika kwenye viwanja vya wazi vya ofisi ya Mkuu wa Mkoa huku tahadhari zote za kuenea kwa ugonjwa huo zikizingatiwa.
Akikabidhi msaada huo Meneja wa CRDB Kanda ya Kusini Bi, Jenifer Tondi Amesema Benki ya CRDB inathamini jitihada zinazofanywa na serikali katika kupambana na ugonjwa huu na hivyo wameona umuhimu wa kuongeza nguvu ili kutokomeza janga hili.
“CRDB tukiwa kama jamii ya wanamtwara tunawajibika moja kwa moja kushirikiana na serikali katika jitihada za kuzuia maambukizi, hivyo tumeona tuongeze nguvu katika kile tulichojaliwa” Amesema Jenifer.
Akipokea Msaada huo Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa amesema msaada huo ni muhimu sana kwa wananchi wa Mkoa wa Mtwara hasa katika kipindi hiki ambacho serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha inawakinga wananchi dhidi ya ugonjwa huu. Aidha ameagiza msaada huo uelekezwe kwa waendesha Pikipiki maarufu kama Bodaboda. Amesema Bodaboda ni kundi mojawapo katika jamiii ambalo linafanya shughuli nyingi na lipo kwenye Hatari ya kuambukizwa hivyo wanapaswa kukingwa na maradhi haya.
“Kuna maeneo ambayo yanachangamoto. Na kwa msaada huu nauelekeza kwenye vituo vya Bodaboda. Bodaboda wanachukua abiria wengi lakini wengi wao hawajachukua tahadhari ya kunawa. Kupitia Msaada huu vituo vingi vya Bodaboda hasa vilivyoko ndani ya manispaa watakuwa na chachu ya kuchukua tahadhali YA kujikinga na ugonjwa huu hatari.” Amesema Byakanwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.