Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed amewaagiza wataalamu wa Halmashauri ya Mji wa Masasi kuhakikisha wanafanya tathmini ya kina ya vyanzo vyao vya mapato na kuitumia taarifa watakayoipata kubuni vyanzo vipya hatua ambayo amesema itasaidia kuijengea Halmashauri uwezo wa kutekeleza miradi yake ya maendeleo kwa tija na kuondokana na utegemezi.
Kanali Abbas ametoa kauli hiyo katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Masasi ikiwa ni siku ya pili ya vikao vya mabaraza maalum ya kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) na kusisitiza kuwa endapo Halmashauri zitaweka mfumo mzuri wa kudhibiti vyanzo vyake vya mapato ya ndani na kurekebisha kasoro zitakazobainika itasaidia kupunguza kasi ya upotevu wa mapato ya Serikali.
“Ndugu wajumbe wa kikao hiki, ni dhahiri kuwa si rahisi kujirekebisha bila kuyagundua mapungufu yako, hivyo ninawaagiza wataalamu kuweka udhibiti katika mashine za kukusanyia mapato (POS) pia wahakikishe wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara kama njia ya kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali.” alisema kanali Abbas.
Maagizo hayo ya Mkuu wa Mkoa Kanali Abbas yanajibu taarifa ya mweka hazina wa Halmashauri ya Mji wa Masasi Donasiano Mgozi ambaye alimweleza kuwa Halmashauri hiyo imetuma miamala ya mapato kimakosa yenye thamani ya Shilingi 130,978,769.97.
“Ndugu wataalamu, haya makosa tumeelekezwa namna ya kuyarekebisha kisheria, mnashindwaje kufuata maelekezo hayo Ili hoja ifutwe, Sasa ninawaagiza nendeni mkakamilishe taratobu za kisheria kama, sitarajii kukutana na hoja ya aina hii tena katika vikao vyetu vijavyo” alisisitiza kanali Abbas.
Halikadhalika katika jitihada za kupunguza hoja za CAG Kanali Abbas ameiagiza Halmashauri hiyo, kuweka mfumo mzuri wa marejesho ya mikopo inayotolewa kwa vikundi, kutumia mifumo na Sheria za manunuzi kama ilivyoelekezwa kwenye miongozo pamoja na kutenga na kuitumia asilimia 40 ya fedha za maendeleo kama ilivyoelekezwa.
Pia kufuatia taarifa ya hoja ya kukosekana kwa hati miliki ya Hospitali ya Mkomaindo iliyojengwa kwa zaidi ya miaka 50 iliyopita, Kanali Abbas amewaagiza wataalamu hao kutengeneza mifumo ya ndani ya udhibiti wa mali za umma kama njia ya kuepukana na migogoro isiyo ya lazima.
Akihitimisha hotuba yake kwa wajumbe wa kikao hicho Kanali Abbas ameiagiza Halmashauri hiyo kutoa mafunzo stahiki kwa watumishi wa idara ya Afya kuhusu utaratibu wa kujaza fomu za malipo ya wagonjwa na kusema kuwa haridhishwi na kasi ya utendaji katika eneo hilo.
“Ndugu wajumbe taarifa niliyonayo inaonesha fedha nyingi katika sekta ya Afya inapotea kutokana na ujuzi mdogo wa kujaza fomu za madai walionao wataalamu wetu, hivyo ninawaagiza nendeni mkawajengee uwezo kwa kuwapatia mafunzo stahiki ili kuondokana na hoja hii ya upotevu wa mapato” alisisitiza Mkuu wa Mkoa Kanali Abbas.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Masasi Lauteri Kanoni amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa Serikali ya Wilaya itasimamia kikamilifu fedha zote za miradi ya maendeleo zinazotolewa na serikali huku akiwaasa wataalamu wa halmashauri hiyo kuepuka kuweka mbele maslai binafsi .
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, Serikali imekuwa ikituletea fedha nyingi za miradi ya maendeleo ikiwemo fedha za mradi wa BOOST, lakini tumebaini wapo watendaji wachache wasio waaminifu ambao wanatumia visingizio vya Kila aina ili miradi isitekeleke, naomba nikuahidi kupitia kikao hiki sasa tumeamua kuwachukulia hatua” alisisitiza Kanoni.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Masasi, Mariam Kasembe amewataka madiwani kuisimamia kikamilifu Halmashauri hoyo ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
“Ndugu zangu madiwani nafikiri sasa umefika wakati nyinyi wenyewe mkae chini mtafakari ni kwa kiwango gani mmeweza kuwasimamia wataalamu hawa kupunguza dosari katika taarifa ya CAG, kama hakuna majibu ya kutosheleza basi nendeni mkajipange upya ili muweze kuja na majibu yenye tija zaidi siku zijazo” aliongeza Bi Kasembe.
Vikao hivyo vya Mabaraza Maalum ya kujadili hoja za CAG kwa Mkoa wa Mtwara vinaendelea kesho Juni 14,2023 ambapo itakuwa ni zamu ya Halmashauri ya Nanyumbu.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.