Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed Leo hii ameshiriki hafla ya kukabidhi magari ya wagonjwa na ya ufuatiliaji pamoja na pikipiki kwa waheshimiwa wabunge wa Mkoa wa Mtwara.
Kanali Ahmed amesema, Mkoa wetu umepokea jumla ya magari 21 ambapo magari tisa (9) ni kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliji wa shughuli za afya katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya, magari 12 ni ya wagonjwa yaliyogawanywa kwa orodha ya majimbo yetu na yanapelekwa katika hospitali na vituo vya afya vinavyotoa huduma za dharura za upasuaji kwa kina mama wajawazito.
Upatikanaji wa magari mapya 12 ya wagonjwa imetusaidia kupunguza upungufu uliokuwepo hapo awali wa magari 35 hadi 23. Magari haya yakatumike kwa kufuata miongozo sheria, kanuni na taratibu za serikali.
Aidha, hii ni siku muhimu sana katika Mkoa wetu na wananchi kwa ujumla kwani magari haya yanalenga kuimarisha utoaji wa huduma za afya. Mtakumbuka jinsi magari yetu ya usimamizi yalivyokuwa machakavu na kupelekea watumishi wetu kushindwa kufika katika vituo vya huduma za afya. Pia mtakumbuka jinsi ambavyo Serikali yetu imejenga vituo vingi vya afya kwa ajili ya huduma za dharura za upasuaji 24 ambavyo viliongeza mahitaji ya magari ya wagonjwa katika vituo hivyo.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara akaongezea na kusema tutambue juhudi kubwa za waheshimiwa Wabunge wetu katika kuhakikisha Mkoa wetu unapata magari ya kutosha katika sekta ya afya tangu nchi yetu ipate uhuru. Wabunge wetu wametumia ushawishi mkubwa sana na kusimama pamoja kuusemea mkoa wetu siyo katika masuala ya afya tu lakini pia katika sekta zingine za huduma kama maji, umeme, elimu.
Waheshimiwa Wabunge wetu hawa hawakuiacha pembeni sekta ya uzalishaji ambapo mwaka huu tumeshuhudia bandari yetu imesafirisha korosho zilizozalishwa katika mkoa wetu na mikoa ya jirani hali iliyochochea ukuaji wa Uchumi wa mkoa. Waheshimiwa Wabunge tunawasihi muendelee kufanya kazi kwa umoja huu ili kuendelea kuleta fursa nyingine za maendeleo katika Mkoa wetu.
Aidha, Katika miaka hii mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Jemedari wetu Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri wa muungano wa Tanzania, uwekezaji mkubwa umefanyika katika sekta ya afya ambapo Mkoa wetu umejenga hospitali mpya katika Halmashauri 5 na kukarabati hospitali kongwe katika Halmashauri 4, ujenzi wa vituo vingi vya afya kwa ajili ya huduma za dharura za upasuaji kwa kina mama wajawazito, ujenzi wa zahanati katika vijiji. Pia ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa katika vituo vya kutolea huduma za afya. Hatuna cha kumlipa Mhe. Rais zaidi ya kuendelea kumshukuru na kumuombea afya njema katika kutekeleza majukumu yake.
Kanali Ahmed akasisitiza, tuendelee kusimamia utendaji na maadili ya kazi kwa wataalamu wetu wa afya ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Kiutumishi ili kupunguza malalamiko na manung’uniko ya wananchi wetu kwenye sekta ya afya. Pia tuhakikishe tunalipa stahiki za kisheria kwa watumishi hawa ili kuwaongezea motisha na hari ya kutoa huduma kwa wananchi.
Aidha katika Hafla hii ya leo, nakabidhi pikipiki 5 kwa Maafisa ugani wa Mifugo wa Halmashauri ya Mtwara wakiwakilisha Halmashauri zingine 8 kwa ajili ya kuwahudumia wafugaji. Nawaelekeza kwenda kuwahudumia wafugaji pamoja na kuzitunza pikipiki hizo kwa makini na kafuata taratibu zote zinazohusisha kutumia vyombo vya moto.
#TunaifunguaMtwara
#KaziIendelee
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.