Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed amewaonya baadhi ya wafanyabiashara wanaohujumu zoezi la Usafirishaji wa Korosho kupitia bandari ya Mtwara ambapo, amesema kuna viashiria vya hujuma zinazofanywa na watu wenye nia mbaya ya kukwamisha jitihada za Serikali za kukuza pato la Mkoa kupitia zao la Korosho.
Kanali Abbas ametoa kauli hiyo katika ziara yake ya kushtukiza aliyoifanya leo mchana katika bandari ya Mtwara ambapo ameshuhudia msururu wa malori yaliyokua yakisubiri kuingia ndani kupakua korosho na hivyo kulazimika kutoa maagizo kwa wasimamizi wa kampuni za Usafirishaji.
"Ndugu zangu nimeingia ndani, nimetembelea kila eneo hakuna shida, nimekagua makasha nimejionea yapo ya kutosha yanasubiri mzigo uingie upakiwe, ninachotaka kufahamu ni kwa nini ndani hakuna lori linaloshusha mzigo, lakini hapa nje kuna foleni ya aina hii" Alihoji kwa mshangao Kanali Abbas.
Akizungumza kwa Masikitiko Kanali Abbas aliwaeleza wadau wa Usafirishaji waliokuwa wakisubiri kuteremsha mizigo yao kuwa, tayari Serikali imebaini kuna baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakila njama kuhujumu zoezi hilo na kuonya kuwa Serikali ya Mkoa Itachukua hatua kwa yeyote atakayebainika.
“Kuanzia sasa naagiza, Magari yote yaliyoko hapa nje kwenye foleni yaingie ndani mara moja yaanze kushusha mzigo kama kuna mtu anataka kusafirisha Korosho kwa njia ya barabara alete maombi tutayatathimini kama yana mashiko tutaruhusu, hatutaruhusu figisu figisu katika suala kama hili lenye maslahi makubwa kwa Taifa letu” Alisisitiza Kanali Ahmed Abbas Ahmed.
Zoezi la Kusafirisha Korosho kupitia bandari ya Mtwara ni Utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Wakati wa ziara yake ya Mwezi Septemba, 2023 Mkoani hapa, ambapo alisema Serikali inataka Kuona kila mwananchi ananufaika na mnyororo wa thamani katika zao la Korosho.
Aidha mpaka Kufikia Novemba 7, 2023 Jumla ya makasha 335 sawa na tani 8,275.22 zilikuwa tayari zimeandaliwa bandarini hapo zikisubiri kusafirishwa katika nchi Mbalimbali duniani.
Novemba 8, 2023
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.