Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Kenan Sawala amelimwagia sifa na Pongezi Jeshi la Polisi nchini kwa kuendelea kuimarisha hali ya usalama ya Mkoa huo na wananchi kuendelea kufanya shughuli zao katika hali ya usalama na amani.
Amesema vyombo vya ulinzi vimeendelea kuhakikisha Mtwara inakuwa salama na hata wananchi na makundi mengine mbalimbali wanakaribishwa kuja kuwekeza katika mkoa huu ambao ni rafiki kwa uwekezaji katika sekta mbalimbali.
Pia ametoa rai kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kudumisha amani iliyopo umoja na mashirikiano ambayo ni nyenzo thabiti ya maendeleo.
Aidha, Mkuu wa Mkoa Kanali Sawala amewataka askari Polisi kuendelea kuongeza tija na ufanisi katika utendaji kazi na kuwekeza zaidi kwenye falsafa ya Polisi jamii ambayo imesaidia kuimarisha ulinzi na usalama kupitia Wakaguzi Kata hivyo waendelee kuihamasisha jamii kushiriki kwenye vikundi mbalimbali vya ulinzi shirikishi vilivyopo kwenye maeneo yao.
Kanali Sawala pia ametoa wito kwa wananchi kushiriki ipasavyo kwenye chaguzi zinazokuja ikiwemo uchaguzi wa serikali za Mitaa pamoja na uchaguzi Mkuu.
Kanali Sawala ameyasema hayo wakati wa hafla za uvishaji wa nishani kwa maafisa, wakaguzi na askari zoezi ambalo limeongozwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP. Camillus Wambura zilizofanyika katika viwanja vya FFU Mtwara.
Juni 6, 2024.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.