Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara CPA Bahati I. Geuzye, aliongoza kikao cha wadau wa chumvi wa Mkoa wa Mtwara. Kikao hicho kilikuwa na lengo la kujadili changamoto zinazo kwamisha ongezeko la kaya zinazotumia chumvi yenye madini joto ya kutosha katika Mkoa huo na kuweka mikakati ya pamoja. Alifafanua kuwa, agizo la uandaaji wa kikao hicho lilitolewa na Mhe. Kanali Patrick K. Sawala Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kwenye kikao cha Tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kilichofanyika tarehe 03/05/2024.
Aliendelea kueleza kwamba, kaya zinazotumia chumvi yenye madini joto ni asilimia 47 na lengo lililowekwa ni asilimia 90 au zaidi. Changamoto zilizobainishwa kukwamisha ongezeko la kaya zinazotumia chumvi yenye madini joto ya kutosha ni ukosefu wa umeme ya kuendeshea mitambo, uhaba wa masoko, madini joto kuuzwa bei ghali, teknolojia duni ya kuchanganya madini joto kwenye chumvi na uhaba wa barabara za kusafirishia chumvi.
Mkurugenzi Mtendaji kutoka Shirika la Madini la Taifa Bwana Venance B. Mwasse alieleza kuwa, Serikali imepanga kujenga Kiwanda cha chumvi Mkoani Lindi kwenye Halmashauri ya Wilaya Kilwa. Alieleza kwamba, kiwanda hicho kitasaidia Mikoa ya Kusini ambayo ni Lindi na Mtwara kadhalika kitaboresha teknolojia ya uzalishaji wa chumvi kadhalika na kuboresha masoko ya chumvi kwenye Mikoa hiyo. Katibu Tawala wa Mkoa CPA Bahati I. Geuzye alimwelekeza Meneja wa TANESCO Mtwara kuhakikisha wanaandaa kwa haraka mpango wa upatikanaji wa umeme kwenye mashamba ya chumvi ili kuboresha uzalishaji wa chumvi. Aidha, aliwataka wataalamu kuhakikisha wanaimarisha usimamizi na kuwajengea uwezo wazalishaji chumvi ili kuimarisha utaalamu kwenye uchanganyaji wa madini joto na chumvi.
Washiriki wengine wa kikao hicho walikuwa ni Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wakurugenzi Watendaji kutoka Halmashauri ya Wilaya Mtwara na Manispaa ya Mtwara Mikindani, Meneja TBS Kanda ya Kusini, Kamishna wa Madini Kanda ya Kusini, Mkurugenzi Mtendaji kutoka Neel Salt Limited, Meneja SIDO Mtwara, Meneja TANESCO Mtwara, Mwenyekiti kutoka Chama cha Wazalishaji Chumvi Taifa, Wazalishaji wa chumvi kutoka Halmashauri ya Wiaya Mtwara, Maafisa Lishe, Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Afya ngazi ya Mkoa na Halmashauri.
Kikao hicho kilifanyika kwenye Ukumbi wa Boma, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara.
Julai 4, 2024
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.