MAADHIMISHO YA KILELE CHA JUMA LA ELIMU MTWARA YAFANA
Posted on: July 27th, 2024
Serikali imetoa shilingi Bilioni 114.5 ndani ya kipindi cha miaka mitatu kwa Mkoa wa Mtwara kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu Mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala amesema hayo leo katika kilelele cha kuadhimisha wiki ya Elimu Mkoani humo.
Kanali Sawala amesema kati ya fedha hizi, shilingi bilioni 76.6 zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na shilingi bilioni 37.9 kwa ajili ya kugharamia elimu ya msingi bila malipo.
Amesema kutokana na fedha hizo na mikakati ya Mkoa ya kuboresha Elimu ambayo iliwekwa na mkoa, mkoa huo umeweza kuboresha elimu na kuleta mafanikio kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo ufaulu kuongezeka.
"Moja ya mikakati ambayo iliwekwa na mkoa ni kuanzisha juma la elimu kwa lengo la kufanya tathmini ya maendeleo ya elimu katika mkoa, kutoa motisha kwa walimu, wanafunzi na Halmashauri pamoja na wadau wa elimu, amesema.
Akizungumzia kuhusu maendeleo ya elimu Mkoani humu, Afisa Elimu wa Mkoa John Lupenza ametaja baadhi ya mafanikio yaliopatikana kuwa ni ufaulu wa wanafunzi ambao wanajiunga na shule za sekondari, kuongeza uwezo wa wanafunzi wa darasala la kusoma , kuandika na kuhesabu.
Katika hafla ya kuhitimisha juma la elimu, serikali ya Mkoa ilitoa zawadi mbalimbali kama motisha kwa walimu, wanafunzi, Halmashauri na wadau ambao wamekuwa wakisaidia mkoa huo katika kuboresha mazingira ya elimu.
Hali kadhalika Kanali Sawala amemkabidhi tuzo ya Shukrani kwa Mdau wa Elimu na Mgeni Maalum Meja Jenerali Marko Elisha Gaguti kwa kutambua na kuthamini mchango wake katika kukuza sekta ya Elimu mkoani Mtwara.