Changamoto ya usafiri kwa Maafisa Tarafa wa Mkoa wa Mtwara imepata ufumbuzi baada ya Serikali ya Mkoa kuwanunulia pikipiki. Pikipiki hizo 20 ambazo zimegawiwa leo kwa walengwa zimegharimu shilingi milioni 48 ambazo zimepatikana baada ya Serikali ya Mkoa kutenga fedha hizo katika bajeti yake ya mwaka 2017/2018. Akizungumza juu ya upatikaji wa pikipiki hizo wakati wa zoezi la kuwakabidhi walengwa lililofanyika leo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Alfred Luanda amesema idadi hiyo ya pikipiki inawafanya Maafisa Tarafa wote waliopo kwa sasa kufikiwa.
Awali akikabidhi pikipiki hizo Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Byakanwa amewataka Maafisa Tarafa kufanya kazi kwa kujituma na kwamba Serikali inawathamini. Aidha, amewataka wahakikishe wanazitunza kwa kuzifanyia matengenezo ya mara kwa mara ili zidumu na kutimiza malengo yaliyokusudiwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Maafisa Tarafa, Octavian Lyapembile wa Tarafa ya Mikindani pamoja na Marko Mapunda wa Tarafa ya Mangaka Nanyumbu wamesema wamepokea vyombo hivyo vya usafiri kwa furaha na kwamba Serikali itegemee mabadiliko chanya ya utendaji kazi. Wanasema walikuwa na changamoto kubwa ya usafiri kutokana na ukubwa wa maeneo yao ya Utawala jambo ambalo lilikuwa likiwalazimu kutembea kwa miguu kwa umbali mrefu na kusababisha kutokufikia maeneo yao ya utawala kwa wakati hivyo kufanya utendaji kazi kuwa mgumu. Kwa kupatikana kwa vyombo hivyo sasa kazi imekuwa nyepesi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.