Jamadi Omari na Evaristy Masuha.
Ujenzi wa miundombinu ya Kituo cha Afya Likombe umefikia asilimia 93 ukiwa umegharimu milioni 326,457,759.18. Kati ya milioni 500 zilizotolewa na serikali kuu kwa kazi hiyo.
Asilimia 7 iliyobaki inatarajia kukamilika baada ya wiki mbili kuanzia Januari 1, mwaka huu. Hadi kukamilika mradi huo Manispaa imekadiria kutumia milioni 400 na kubakiwa na shilingi milioni 100.
Akizungumza kwenye ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa mradi huo iliyofanyika Januari 1, 2018 kati ya Timu ya ukaguzi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Timu ya Menejiment ya halmashauri, Mkurugenzi wa Manispaa Bi Beatrice Dominic amesema Ujenzi huo unaendelea vizuri na kwamba fedha zitakazobaki zitatumika kukamilisha miundombinu mingine katika kituo hicho ikiwemo ukarabati wa jengo La OPD na Ujenzi wa choo cha wagonjwa.
Kuhusu mikakati iliyotumika katika ujenzi huo hadi kupelekea kukisia kubakiwa na fedha Beatrice amesema kuwa Ofisi yake imetii agizo la Serikali lililotaka mradi huo kujengwa kwa kutumia mafundi wenyeji ambao wametoa gharama za ujenzi zilizo halisi na kazi imekuwa nzuri,na kwamba kila jengo amepewa fundi mmoja na vibarua wake.
Ameongeza kuwa Menejimenti ya halmashauri ilikubaliana vifaa vyote vya ujenzi vinunuliwe viwandani ikiwemo mabati,Gypsum,Tiles,rangi,cable za umeme na vifaa vingine ili kuweza kupunguza gharama na vifaa vichache vilinunuliwa kwenye eneo la Manispaa pamoja na mafundi waliojenga majengo hayo.
Aidha amesema kuwa mradi umefikia hapo kwa kuwa kulikuwa na umakini mkubwa kwenye usimamizi na kwenye kufanya makadirio Lakini pia ushirikiano ulikuwa mkubwa kati ya timu ya halmashauri na Timu ya uendeshaji wa kituo.
Kwa upande wake Kiongozi wa Timu ya Mkoa ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu, Duncan Thebas amepongeza Manispaa kwa kazi nzuri iliyofanyika na kwamba inadhihirisha maamuzi sahihi ya Serikali ya kuikomboa Tanzania kwa kutumia mafundi wenyeji kwenye ujenzi wa miundombinu hiyo. Aidha amepongeza ujenzi wa njia za kupita (walk way) ambayo kwenye maelekezo ya mradi haikuwepo lakini Manispaa imeona umuhimu wa kuijenga.
Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa DR.Christa Nzali ameishukuru Serikali kwa kuleta fedha hizo kwani kukamilika kwa majengo hayo kutasaidia kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo kupunguza vifo vya akina mama na watoto, pia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali ya Mkoa.
Wakati huo huo Fundi aliyepewa kazi ya ujenzi wa Wodi ya Mama na Mtoto Athumani Bandiko ameishukuru Serikali kwa kuwapatia kazi ya ujenzi kwani imewapa nafasi ya wao kuonesha uwezo wao kama mafundi wadogo lakini pia imesaidia kutengeneza ajira kwa vijana. Aidha ameiomba Serikali iwaamini na iendelee kuwapa kazi katika majengo mengine.
Manispaa Mtwara-Mikindani Oktoba 13, 2017 ilipokea fedha kiasi cha shilingi milioni 500 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya afya katika Kituo cha Afya Likombe. Miundombinu iliyojengwa ni pamoja na Wodi ya Mama na Mtoto, Maabara, Chumba cha kulaza Maiti, Chumba cha Kufulia nguo, Kichomea taka pamoja na ujenzi wa Nyumba ya Mganga.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.