Mkuu wa mkoa wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema serikali ya Mkoa haitokubali visingizio vya aina yeyote vinavyolenga kudhoofisha jitihada za serikali za kusafirisha korosho nje ya nchi kupitia bandari ya Mtwara.
Kanali Abbas ametoa kauli hiyo mbele ya Mkuu wa mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack aliyefika mkoani Mtwara kujionea namna zoezi la usafirishaji wa korosho kupitia bandari linavyotekelezwa.
Katika ziara hiyo Mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed amewaeleza viongozi kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara kuwa mkoa wa Mtwara umesimamia kikamilifu utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa asilimia mia moja na kuongeza kuwa kupitia zoezi hilo mamia ya wananchi wamenufaika kiuchumi.
Akizungumza mara baada ya kukagua zoezi la kuteremsha makasha matupu na kupakia makasha yenye shehena ya korosho kwenye meli inayojulikana kama CMA CGM KAILAS Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack amesema wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa vinara wa kutoa taarifa zenye utata ambazo zimechangia kupunguza kasi ya utekelezaji wa zoezi hilo.
“Mhe. Mkuu wa Mkoa, binafsi nimekua nikipata malalamiko kutoka kwa baadhi ya wadau kuhusu suala la miundombinu katika bandari ya Mtwara, wengine wamenilalamikia kuhusu uhaba wa makontena, weninge wanasema eti hakuna meli za kutosha na wengine wameenda mbali zaidi wakasema kuna foleni kubwa sana” alisema kwa mshangao Mhe. Telack.
“Ndugu zangu baada ya ziara yangu bandarini hapa nimebaini kuwa kauli zote zilizotolewa na watu hao ni visingizio vinavyolenga kuupotosha umma kuwa zoezi hili limekosa Ufanisi” aliongeza Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack.
Aidha Mhe. Telack akiwa bandarini hapo ameweza kujionea makasha tupu 1800 yakisubiri kupakiwa korosho ambapo ametoa wito kwa wafanyabiashara na wasafirishaji wenye nia ya kusafirisha mizigo yao kupitia bandari ya Mtwara kufuata utaratibu badala ya kutengeneza visingizio ambavyo vina lenga kuishawishi mamlaka kuruhusu usafirishaji wa korosho kwa njia ya Barabara.
Kwa upande wake meneja wa bandari ya Mtwara Fredinand Nyathi amewahakikishia wakuu wa mikoa ya Lindi na Mtwara kuwa bandari ina miundombinu rafiki na ya kisasa inayoruhusu zoezi la kupakia na kupakua mizigo kufanyika kwa muda mfupi.
Aidha Nyathi ameongeza kuwa hivi karibuni bandari ya Mtwara inatarajia kupokea meli zaidi ya 5 zitakazoleta makasha tupu na kuchukua makasha yenye shehena ya korosho huku kampuni za PIL, CMA na MSC zikiwa tayari zimethibitisha kuleta Meli zake katika bandari ya Mtwara.
Hali-kadhalika Nyathi amewaomba wakuu hao wa mikoa ya Lindi na Mtwara kuendelea kuwahamashisha wafanyabiashara na wasafirishaji kuitumia bandari hiyo kama njia kuu ya usafirishaji wa mizigo ya Korosho na bidhaa nyingine.
Katika ziara hiyo pia wakuu wa Mikoa ya Lindi na Mtwara waliishuhudia meli ya kwanza inayojulikana kama CMA CGM KAILAS ikikamilisha zoezi la kupakia makasha 51 ya korosho baada ya kuteremsha makasha tupu katika bandari hiyo ikiwa tayari kuanza safari kuelekea nje ya nchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.