Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kanali Ahmed Abbas Ahmed leo hii amefungua rasmi kikao cha kamati ya afya ya Msingi (PHC) katika ukumbi wa Boma Ulioko katika ofisi yake Mkoani Mtwara.
Aidha ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya, OR- TAMISEMI na Wadau wa chanjo ambao wamekuwa ni sehemu ya kufanikisha upatikanaji wa chanjo mbalimbali zinazotolewa kwa watoto chini ya miaka mitano (5) na makundi mengine hapa Nchini. Hali hii inaonesha Serikali inavyowajali na kuwakinga Wananchi wake dhidi ya maradhi mbalimbali ikiwemo magonjwa ya milipuko yanayozuilika kwa chanjo.
Kanali Ahmed amesema Halmashauri zetu kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na wadau mbalimbali zimekuwa zikitoa chanjo kwa watoto wote wenye umri wa chini ya miaka mitano dhidi ya magonjwa mbalimbali kama vile Kifua Kikuu, Dondakoo, Kifaduro, Homa ya ini, Kuhara, Vichomi, Homa ya Uti wa mgongo, Kupooza, Surua na Pepopunda. Hii ni katika harakati za kupunguza vifo vitokanavyo na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.
Hapa nchini mafanikio ya chanjo yameonekana dhahiri, kwa mfano tumefanikiwa kutokomeza ugonjwa wa Ndui; magonjwa ya Dondakoo, Kifaduro, Polio na Pepopunda. Mafanikio haya makubwa yametokana na kuwapatia chanjo kwa zaidi ya asimilia 90 watoto walio na umri wa chini ya mwaka mmoja hapa nchini.
Pia nazipongeza Halmashauri zetu kwa kuendelea kufanya vizuri katika kufikia malengo ya kitaifa katika utoaji wa huduma za chanjo za kawaida kwa zaidi ya asilimia mia moja na ufuatiliaji wa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo kwa mwaka 2023 amesisitiza Mkuu wa Mkoa.
Kanali Ahmed ametoa wito, kuwa kila mmoja wetu anao wajibu wa kuhakikisha mtoto wake, mtoto wa jirani au mtoto yeyote yule anapatiwa chanjo ili kuzuia asipatwe na maradhi yanayozuilika kwa chanjo na asiwe hatari kwa wengine kwa kusababisha milipuko.
Kanali Ahmed amesisitiza kuwa Kupitia Kampeni ya Chanjo ya Surua kwa mwaka huu 2024, Mkoa wetu unalenga kuwafikia na kuwapatia chanjo ya surua rubella watoto wenye umri chini ya miaka mitano (Miezi 9-59) wapatao Laki moja sabini na mbili elfu na sitini na mbili (172,062). Uzoefu wa kampeni zilizotangulia unaonesha kwamba mara zote tumevuka malengo tuliyojiwekea kwani idadi hii ni makisio tu na siyo idadi kamili ya watoto wote waliopo kwenye jamii. Hivyo twende tukatekeleze kampeni hii kwa mbinu zote ili tumfikie kila mtoto na siyo tu kufikia lengo.
Aidha Kampeni hii itafanyika kwa utaratibu wa kupitia vituo vya kutolea huduma za Afya, maeneo maalum yenye mikusanyiko ya watu wengi kama vile:- Nyumba za ibada, shule za awali, vituo vya kulelea watoto wadogo mchana, makao ya watoto, stendi za mabasi, masoko, minada na Ofisi ya serikali za Mitaa/Vijiji.
Februari 14, 2024.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.