Timu ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara imeshindwa vibaya na Timu ya jeshi la Polisi Mtwara katika mashindanio ya kujaza maji kwenye ndoo.
Mashindano hayo yaliyofanyika wakati wa Tamasha la “Msangamkuu Beach Festival “2018 timu ya Sekretarieti ya Mkoa ilipata nafasi hiyo baada ya shabiki wake Mkuu Benaya kapinga (Katibu Tawala wilaya ya Tandahimba), kucheza faulo.
Shindano hilo lililokuwa likiwataka washiriki kujaza maji kwenye ndoo ndogo kwa kupokezana mgongoni lilianza kwa mbwembwe huku mchezaji namba moja wa timu ya Sekretarieti ya Mkoa Mhe. Gelasius Byakanwa (RC) akionesha umahiri katika mbio za kuyafuata maji baharini. Hata hivyo mchezaji huyo alionesha udhaifu wa kumpasia mchezaji aliyekuwa mgongoni kwake Dkt.Jilly Maleko (RAS) hali iliyosababisha maji mengi kuishia mgongoni kwake.
Mchezaji pekee aliyeonekana kuimudu vema nafasi yake katika shindano hili ambalo lilikuwa likifanyika kwa mara ya kwanza mkoani hapa ni Mhe.Evod Mmanda (Mkuu wa Wilaya ya Mtwara), ambaye alionekana kuwa mwepesi kumwaga maji na kukimbia kuchota mengine.
Dalili za kushindwa kwa timu ya sekretarieti zilianza kuonekana mapema baada ya kuanza kuingiza wachezaji kinyemela ambapo Mhe. Sebastian Walyuba (Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba) kuvamia mchezo huo bila taarifa ya refa.
Baada ya kuonekana jahazi la timu ya sekretarieti ya Mkoa linaelekea kuzama ndipo mtumishi wa Sekretarieti ya mkoa Benaya kapinga alijipenyeza katikati ya benchi la ufundi akiwa ameficha maji yaliyokuwa kwenye chupa ya maji ya Kilimanjaro.
Hata hivyo Refa alishtukia ujanja huo wakati mchezaji huyo akiongeza maji hayo kwenye ndoo iliyokuwa imeshikiliwa na Dkt Jilly Maleko(Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara).
Pamoja na jitihada hizo bado ndoo ya timu ya Polisi ilikuwa imeshajaa hali ambayo ilimfanya refa apulize kipenga cha kumaliza mchezo na kumpa nafasi Mkuu wa Mkoa amtangaze mshindi.
Akizungumzia hali hiyo Kapinga amemlalamikia refa kwamba hakuwa makini kwani yeye aliamua kufanya hivyo baada ya kuona wapinzani wao wakifanya hivyo.
“Mimi nimewaona wenzangu wanafanya hivyo hivyo na mimi nikaamua kujibu mapigo. bahati mbaya mimi wameniona lakini mwenzangu hakuonekana”. alisema kapinga.
Kwa upande wake Kocha wa timu ya Sekretarieti ya Mkoa Aziza Mangosongo (Mkuu wa Wilaya ya Newala), ameshukuru kikosi chake na kwamba wanaenda kujiandaa kwa ajili ya tamasha la aina hii ambalo limeonekana kuwavutia wengi.
Aidha, Mhe.Mangosongo amemtetea shabiki wake kwamba mchezo ni mbinu, bahati mbaya mbinu yao imeshtukiwa wakati wenzao wakifanikiwa.
Tamasha la “Msangamkuu Beach festival”limefanyika huku likishuhudiwa na umati mkubwa wa wananchi. Tamasha hilo ambalo limefanyika kwa mara ya kwanza limejumuisha michezo mbalimbali ikiwemo Beach soka, michezo ya watoto, mieleka, kuimba. kucheza, kuogelea na kupiga kasia na mingine mingi.
Video yake hii HAPA
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.