Mkoa wa Mtwara uko tayari kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19. Baadhi ya mambo muhimu yaliyozingatiwa katika maandalizi ni pamoja na kutoa elimu sahihi juu ya ugonjwa huo, Kukamilisha mapema Maandalizi ya vifaa muhimu kwa ajili ya kuchukulia sampuli za wagonjwa (tripple packages & VTM), Kutambua maeneo muhimu ambako wahisiwa wa ugonjwa huo watafikishwa, kuwaandaa wataalamu wa maabara. Pia vifaa tiba na dawa muhimu kwa ajili ya kutibu mgonjwa wa aina hiyo vipo.
Hayo yamebainishwa leo Machi 27 na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa ambaye pia ni Mratibu wa Maabara Mkoa, Edward Ngonyani katika kikao maalumu kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Gelasius Byakanwa kwa ajili ya kupeana elimu maalumu juu ya ugonjwa huo.
Amesema elimu ambayo imekuwa ikitolewa ni pamoja na jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo, dalili zake pamoja na hatua za kuchukua inapobainika kuwa na dalili za ugonjwa. Aidha mkoa umetenga vituo vitano kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa watakaobainika kuwa na ugonwa wa COVID-19. Vituo hivyo ni Kituo cha Afya Kilambo ambacho kiko wilaya ya Mtwara, Mkunya ambacho kiko Newala, Mtambaswala kiko Nanyumbu, Mbonde ambacho kiko Masasi pamoja na Majengo.
Naye Afisa Afya Mkoa Sasita Shabani amewataka wananchi wa Mkoa wa Mtwara kuchukua tahadhali hasa kutokana na jiografia ya mkoa Mtwara ambao unapakana na nchi ya msumbiji ambayo pia imegundulika kuwa na wagonjwa wa aina hiyo. Amesema ugonjwa huo unasambaa kwa kasi iwapo tahadhali haitachukuliwa. Amewataka kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola inapobainikika kuwepo na mgonjwa mwenye dalili hizo huku akisisitiza wananchi wasitowe taarifa ambazo hazijapitishwa na mamlaka za serikali na wataalamu wa afya.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Mhe. Gelasius Byakanwa akasisitiza utoaji wa taarifa sahihi ambazo haziwatii hofu wananchi. Amesema hatua zilizochukuliwa na serikali ya Tanzania katika kupambana na ugonjwa huu ni sahihi hivyo zinapaswa kufuatwa. Amewataka wananchi waendelee na shughuli zao huku wakizingatia taratibu za afya.
Kikao hiki kimefanyika Ukumbi wa Chuo cha Uganga (COTC) kikiwahusisha Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa, Waganga Wakuu wa Wilaya, wakuu wa Taasisi za serikali na Binafsi pamoja na viongozi wa Dini ikiwa ni mwendelezo wa vikao vyenye lengo la kutoa elimu juu ya ugonjwa wa COVID-19 ulioanzia nchini China mwishoni mwa mwaka jana.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.