Picha ya pamoja ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt John pombe Magufuli na viongozi mbalimbali wa serikali mara alipotembelea mkoani Mtwara Machi 4, 2017
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Halima Dendego amewaongoza mamia ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara katika Hafla fupi ya Kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Katika Hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Kanisa Katoliki Mtwara jana Mheshimwia Dendego amemsifu Mheshimiwa Magufuli kwa kusimama kidete katika kusimamia rasilimali za Tanzania. Amesema uamuzi wake wa kuzuia usafirishaji wa makinikia nje ya nchi na hatimaye kuunda tume zilizoleta majibu ya upotevu mkubwa wa rasilimali za Tanzania ni wa kupongezwa na kila Mtanzania mwenye nia njema na nchi yake.
Dendego ambaye alihudhuria tukio la uwasilishaji wa taarifa ya Tume ya pili iliyoongozwa na profesa Osolo amesema Rais aliongea kwa hisia kubwa ikionesha ni jinsi gani asivyo na mzaha katika mapambano makubwa kuhakikisha rasilimali za watanzania zinawanufaisha watanzania.
Ameeleza kuwa watu wenye nia ovu tunao katika ofisi zetu hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kwa nafasi yake kuhakikisha anapambana na watu wa aina hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mheshimiwa Evod Mmanda amemtaka Mheshimiwa Magufuli kutoyumbishwa na kelele za watanzania wasioitakia mema nchi yetu.
Amesema Tume zote mbili zilizoundwa kufuatilia sakata hilo zilijumuisha watu makini waliobobea katika masuala husika, hivyo walichokibaini ni kitu cha kupigiwa makofi na kupewa ushirikkiano wa dhati katika kupata ufumbuzi.
Katika tukio hilo lililopambwa na kwaya ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tawi la Mtwara, wananchi katika makundi mbali ya kijamii walitoa salamu zao kwa Mheshimiwa Rais wakimtakia mapambano hadi mwisho wa vita.
Akiwasilisha salamu za wazee, kupitia mwamvuli wa Chama cha Wastaafu na Wazee Mkoa wa Mtwara, Mzee Caspar Zenda amesema Taarifa ya Profesa Nehemiah Osoro kuhusu usafirishaji wa makinikia nje ya nchi iliwashtua na kuwahuzunisha sana. Hivyo wanampongeza Rais kwa hatua alizozichukuwa dhidi ya hao waliofanya kitendo hicho cha kifisadi. Wanasema waliofanya hivyo ni mafisadi wakubwa na kwamba wazee wa Mtwara wanawalaani kwa nguvu zote.
‘Baba wa taifa letu hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambaye alikuwa Rais wa kwanza wa Tanzania, mara kwa mara katika hotuba zake kwetu wananchi alisisitiza umuhimu wa vitu vinne ambavyo ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora kuwa ni msingi wa maendeleo ya taifa letu.
Hayo yote yalizingatiwa na viongozi wote walioongoza taifa letu kwa nyakati mbalimbali, hasa katika awamu hii ya tano katika uongozi wako unasimamia kwa dhati zaidi na matokeo yake tunayaona. Tumefurahi na kufarijika sana. Unafanya juhudi kubwa kuboresha Maisha ya wananchi wote kwa kusisitiza matumizi mazuri ya raslimali zetu nchini’. Walisisitiza wazee.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoani Mtwara, Hassan Simba kwa niaba ya waandishi wenzake amesema Tanzania inazo rasilimali nyingi ambazo zinahitaji usimamizi makini ili kukuza uchumi wa nchi.
‘Nchi yetu ya Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi zikiwemo madini, gesi asilia, mafuta, maziwa, mito, mbuga za wanyama zenye kuchochea Utalii na Uwekezaji ambazo zote hizi zinahitaji usimamizi wa viongozi waadilifu. Tuna imani na wewe Rais. Tunakuombea Kwa Mungu uvishinde vita hivi.
Mapema mwaka huu Rais aliounda Tume mbili tofauti kufualtilia thamani ya madini yaliyoko kwenye 277 ya Makinikia aliyoyazua bandarini ambapo tume ya pili iliyundwa chini ya Mwenyekti Profesa Nehemiah Osoro ilibaini hasara ya zaidi ya Shilingi trilioni 183.597 hadi trilioni 229.977 kiwango cha juu tangu yaliporuhusiwa kusafirishwa nje ya nchi mwaka 1998 uamuzi ambao umekuwa ukipongezwa na makundi mbalimbali katika jamii.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.