Kuelekea miaka 19 bila Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere wakazi wa Mtwara Mikindani wameiomba serikali kukarabati nyumba aliyofikia mwalimu Nyerere wakati wa harakati za mapambano ya uhuru. Nyumba hiyo iliyojengwa na Mahajub Mahamoud mmoja wa wanajeshi wa jeshi la Mkoloni imekuwa gofu na kuta zake zimeanza kudondoka.
Akizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii wakati wa uzinduzi wa Mji Mkongwe wa Mikindani mapema mwezi huu Mzee Mohamed Kidume ambaye ni moja ya wazee maarufu mjini Mikindani amesema kwa wakati huo nyumba hiyo iliyoko ndani ya hifadhi ya mji Mkongwe wa Mikindani ndiyo nyumba iliyoonekana kuwa na hadhi ya kulala mgeni maarufu kama mpigania uhuru wa Tanganyika mwalimu Julius kambarage Nyerere. Pamoja na umaarufu huo nyumba hiyo imetekelezwa na sasa inaelekea kuanguka.
“Jambo ninalosikitika ni kwamba chama hakitaki kutengeneza hii nyumba, na serikali haitaki kusaidia vilevile. Leo umekuja umekuta zile kuta. Atakapokuja mtu mwingine atakuta huo ukuta haupo. Tafadhali nyumba inakufa na tutakuwa hatuna faida yoyote. Amesema Mzee Kidume”.
kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Japhet Hasunga amepokea ushauri huo na kumuagiza katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Aloyce Nzuki kuhakikisha nyumba hiyo inakarabatiwa na kukamilika ndani ya mwaka mmoja.
“…na nyinyi kama Wizara ile ya Mwalimu muisimamie. Nawapa mwaka mmoja mhakikishe mmeikarabati yote na imekamilika”.
Akilezea historia ya ujenzi wa Nyumba hiyo Mzee Kidume amesema ilijengwa na Mtanzania aliyejulikana kwa jina la Mahamoud ambaye alikuwa askari wa jeshi la mkoloni makazi yake yakiwa Dar es Salaam.
Aidha ujenzi huo ulikuwa ukisimamiwa na kaka yake aliyejulika kwa jina la Ahmed Adam wakati huo Mahamoud akituma fedha kutokea Ujerumani alikokuwa vitani.
hata hivyo Mahamoud hakuweza kuiona nyumba hiyo kwani alifariki akiwa vitani.
Video yake hii HAPA
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.