Kiongozo wa Mbio za Mwenge kitaifa Amour Hamad Amour, amewataka wananchi mkoani Mtwara kupanda miti ili kuhifadhi mazingira. Amour ameyasema hayo leo Wakati akizindua mradi wa shamba la miti la mjasiliamali Joseph Kamkumba lililoko kijiji cha Mchemo Wilayani Newala.
Amesema miti ina umuhimu mkubwa katika kutunza na kuhifadhi mazingira na kuyafanya yaendelee kuwa katika uhalisia. Bila kufanya hivyo mazingira yatapoteza uhalisia na kuchochea majanga mbalimbali yakiwemo majanga ya ukame.
Katika kusisitiza suala hilo amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Newala Mheshimiwa Azizi Mangosongo kuhakikisha anasimamia zoezi hilo na kulifanya shamba la miti la Kamkumba kuwa shamba darasa.
‘Miti ina umuhimu mkubwa katika maisha ya binadamu kwani inasaidia kuzuia upepo ambao ungeweza kuleta madhara katika makazi ya watu. Pia inatunza mazingira na kuyaweka katika uhalisia’. Amesema.
Amour ambaye anaendelea na mbio za Mwenge Mkoani Mtwara kwa siku ya Nne sasa ametoa pongezi kubwa kwa viongozi wa Wilaya na Halmashauri Wilaya ya Newala na kuwataka waendelee na usimamizi wa masuala ya kilimo ili wasaidie wananchi kuyafikia malengo yao.
Kwa upande wake Afisa Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Magreth Likonda amesema shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 17, miti 5,000 lilianzishwa mwaka 2011 baada ya kupata ushauri kutoka halmashauri.
Baada ya kuanzisha shamba hilo ambalo amekuwa akilipanua kila mwaka limeonesha manufaa ambapo mwaka 2013 Mwenge wa uhuru ulitembelea shamba, likakaguliwa na kupanda miti.
Likonda ameyataja manufaa ya mradi huo kuwa ni pamoja na kuhifadi mazingira, na kukabiliana na upungufu wa mazao ya misitu. Pia kutengeneza ajira kwa wakazi wa eneo hilo. Aidha shamba hilo pia linatumika kama amana kwa kukopa mikopo Benki.
Kwa upande wake mmiliki wa shamba hilo, Joseph Kamkumba ameshukuru Mwenge wa uhuru kukagua shamba hilo na kuahidi kuongeza jitihada zaidi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.