Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Brig. Jenerali Marco E. Gaguti amekabidhi Mwenge wa Uhuru leo kwa RC wa Mkoa wa Ruvuma Brig.Jener. Wilbert Augustine Ibuge kwenye kijiji cha Sautimoja kata ya Namakambale, Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma
Akizunguma wakati wa makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru, RC Gaguti amesema kuwa Mwenge huo maalumu wa Uhuru unaokimbizwa na vijana 6 wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), umepita Mkoani Mtwara na kutembelea, kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya Msingi kwenye miradi 42 yenye thamani zaidi ya sh. bilioni 11 mkoani humo.
Aidha, Gaguti amesema kuwa wakati wa mbio hizo jumla ya Wananchi 492 walipima Malaria wanaume 338 na wanawake 492 na waliogundulika kuwa na Malaria ni 40, Wananchi 1619 walijitokeza kupima VVU wanaume wakiwa 920 na wanawake 699 na kati yao 7 walibainika kukutwa na virusi 4 wakiwa wanawake na 3 wanaume , Pia uchangiaji wa damu ulifanyika na jumla ya vyupa 96 za damu zilipatikana.
Mhe. Gaguti amesema kuwa Mwenge wa Uhuru ukiwa mkoani humo, viongozi walihamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kupata chanjo kwa ajili ya kujikinga na janga la Corona.
Amewapongeza wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa wakiongozwa na Josephine Mwampashi kwa kazi kubwa waliyoifanya wakiwa mkoani humo na kuahidi kuzifanyia kazi kasoro chache zilizojitokeza katika miradi miwili (2) na kuhaidi kuzirekebisha.
RC Gaguti amewashukuru wakimbiza Mwenge wa Mkoa huo pamoja na viongozi na wananchi kwa kushiriki vyema wakati wa mbio hizo za Mwenge na kumaliza salama.
Kwa upande wake Kiongozi wa wakimbiza Mwenge wa Uhuru Josephine Mwampashi ameshukuru kwa ushirikiano walioupata wakiwa Mkoani humo na kusema kuwa Mwenge wa uhuru ulipita kwenye miradi mbalimbali katika kuleta chachu ya maendeleo na kusisitiza kuwa watekelezaji wa miradi wakasimamie kizalendo ili kuleta maendeleo katika Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Pichani; Kiongozi wa mbio Maalum za Mwenge
wa Uhuru Josephine Mwampashi wakati akiuaga
Mkoa wa Mtwara Kuelekea Mkoani Ruvuma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.