Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Byakanwa akionesha moja ya nyumba ya Mwalim ambayo marekebisho ya nyavu za madirisha hazijafanyika jambo ambalo lilimsikitisha na kuwataka walimu kuzijali na kuzitunza nyumba hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Byakanwa ameagiza walimu wote mkoani Mtwara waliopewa nyumba za kuishi kuingia mikataba na Halmashauri kwa ajili ya utunzaji wa nyumba hizo.
Agizo hilo amelitoa jana wakati akikagua nyumba za walimu wa shule ya msingi Lulindi 1 iliyoko kijiji cha Muungano kata ya Lulindi Wilayani Masasi mara baada ya uzinduzi wa zoezi la upandaji miti kimkoa lililofanyika kijijini hapo.
Mheshimiwa Byakanwa amesema hatavumilia mwalimu anayepewa nyumba bure kushindwa kuitunza. Anasema ni bora nyumba hiyo akapewa mwalimu mwingine mwenye moyo wa kuitunza kuliko Mwalimu anayesubiri serikali imfanyie kila kitu.
Amesisitiza kuwa serikali imeonesha kujali ndiyo maana imewajengea nyumba na kuwapa waishi bure hivyo haipendezi mwalimu anayeishi katika nyumba hiyo kuendelea kusubiri serikali irekebishe mambo madogomadogo ikiwemo nyavu za madirisha zilizochoka.
Licha ya agizo hilo Mheshimiwa Byakanwa ameahidi kuchangia bati za vyumba vitatu vya madarasa kwa sharti la kuwataka wanakijiji kuhakikisha wanajenga boma. Pia ameitaka serikali ya kijiji hicho kuandaa tofari za kutosha nyumba mbili za walimu ambapo amemutaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Juma Satma kuchangia ujenzi wa nyumba hizo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Juma Satma amesema agizo hilo wamelipokea na kwamba wako tayari kulifanyia utekelezaji.
Awali akiwasilisha kero ya shule hiyo Rajab Abdelimali Soni, mkazi wa kijiji hicho alimuomba Mkuu wa Mkoa kutembelea shule hiyo kutokana na changamoto ya miundombinu ya shule hiyo.
Amesema shule hiyo ni kongwe lakini bado inatatizo la miundombinu ya nyumba za walimu pamoja na vyumba vya madarasa jambo ambalo limekuwa likisababisjha walimu kuishi mbali na mazingira ya shule na hivyo kuathili utendaji kazi.
Kutazama Video yake Bonyeza HAPA
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.