Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa (wa tatu kutoka kulia) akifuatilia jinsi pombe ya mabibo inavyotengenezwa mara alipotembelea wazalishaji wa pombe hiyo katika Kijiji cha Chigugu wilayani Masasi
Akiwasilisha majibu ya Sampuli ya pombe ya mabibo (gongo) iliyotumwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kujua usalama wa kinywaji hicho amesema Mkemia Mkuu amethibitisha kuwa vimiminika hivyo havikukutwa na madini mengine ambayo ni sumu kwa watumiaji.
“Vimiminika vyote vimekutwa na vileo tofafuti kuanzia 8 mpaka 45.9 na ethano au kilevi salama. Havijakutwa na madini mengine ambayo ni sumu kwa madhara ya watumiaji”. Amesema Byakanwa.
Amesema sampuli hizo zilichukuliwa kwa wazalishaji wa pombe hiyo kutoka katika vijiji vya Chigugu wilayani Masasi ambako alichukua sampuli Nne. Kijiji cha Nambeleketela na Majengo vilivyoko wilayani Mtwara alichukua sampuli saba.
“ … na kwa kuwa pombe hizi zilizopimwa zimekutwa salama na hazina madhara. Nimemwandikia waziri wa sheria na Katiba nikimuomba kufanyiwa marekebisho sharia ya pombe za kienyeji ili sheria iruhusu uzalishaji na utengenezaji wa pombe za kienyeji ikiwa ni hatua ya kukuza viwanda na kuongeza thamani ya bidhaa. …nimemwandikia barua waziri wa viwanda nikimuomba atowe ruhusa kwa wanamtwara kuzalisha pombe za kienyeji kwa kutumia mabibo”
Byakanwa amesema Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele kusisitiza utafiti na mara ya mwisho akiweka jiwe la Msingi la ujenzi wa barabara ya Mtwara Tandahimba alisisitiza kufanya utafiti wa gongo itokanayo na mabibo ili kubaini kama inafaa kwa matumizi mbalimbali ya binadamu. Kufuatia agizo hilo Byakanwa aliamua kukutana na wazalishaji wa pombe hiyo ili kupata sampuli ambayo aliiwasilisha kwa mkemia Mkuu wa Serikali.
Aidha amewaagiza wakurugenzi wote wa halmashauri za mkoa huo kuwasajili na kuwatambua watengenezaji wote wa gongo.
“Kwa kuwa mkoa unayo fursa ya nzuri ya kuzalisha bidhaa nyingi zitokanazo na mabibo na zitokanazo na gongo. Ninawaagiza wakurugenzi wote wa halmashauri zote kuwasajili na kuwatambua watengenezaji wote wa gongo wakati tukisubiri maamuzi ya waziri wa viwanda ili tutengeneze kanzi data ya wazalishaji na kiwango cha uzalishaji.”
Mafanikio ya zoezi hili yataongeza thamani ya zao la korosho kutoka kwenye mauzo ya korosho ghafi hatimaye kuongeza mauzo ya mabibo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.