Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mheshimiwa Godfrey Zambi akipoka maelekezo ya utendaji wa bandari kutoka kwa afisa wa Bandari
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mheshimiwa Godfrey Uwezo Zambi amewataka wafanyabiashara wa Korosho kuitumia Bandari ya Mtwara kwani ina uwezo mkubwa wa kuhudumia shehena hiyo. Amesema hali ya Bandari ya Mtwara kwa sasa ni nzuri hasa baada ya kutatua changamoto zilizokuwepo mwaka jana. Mheshimiwa Zambi ameyasema hayo jana mara baada ya ziara yake fupi ya kutembelea bandari hiyo.
Amesema mwaka jana aliwaruhusu wafanyabiashara walionunua korosho mkoani kwake kufanya uamuzi wao wenyewe iwapo watatumia Bandari ya Mtwara au Dar es Salaam katika kusafirisha shehena hiyo nje ya nchi kutokana na malalamiko mengi aliyoyapata kutoka kwa wafanyabiashara wenyewe.
Ametaja baadhi ya changamoto kuwa ilikuwa ni pamoja na uhaba wa makasha ya kufungia korosho, eneo la kufanyia kazi hiyo na uhaba wa Miundombinu ya kupakia na kupakua mizigo.
Amesema kwa hali aliyoishuhudia baada ya kutembelea bandari hiyo hana shaka kuwa changamoto nyingi zimeisha na hivyo Bandari inaweza kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Ameupongeza uongozi wa Bandari na serikali kwa ujumla kuamua kufanya jitihada za dhati za kuondoa changamoto hizo.
Awali akiwasilisha taarifa ya Bandari, Mkuu wa Bandari ya Mtwara, Nelson Mnali amesema wamejipanga kuhakikisha changamoto zote zinatatuliwa kwa wakati. Amesema mwaka jana Bandari ilihudumia tani 215,852 ya shehena ya korosho, mwaka huu wamejiwekea malengo ya kuhudumia tani 230,000 sawa na ongezeko la asilimia 6.5.
Amesema eneo la kuhudumia meli ni kubwa kwa sasa hasa baada ya kampuni zilizokuwa zimekodi maeneo ndani ya Bandari hiyo kwa ajili ya kuhudumia kampuni za mafuta ya gesi kumaliza mikataba yao.
Hali hiyo imefanya Bandari iwe na uwezo wa kuhudumia meli mbili kwa wakati mmoja tofauti na mwaka jana ambapo eneo lilikuwa linawezesha kuhudumia meli moja kwa wakati. Pia Bandari imewezesha upatikanaji wa makasha ya kuhifadhia korosho ambapo hadi wakati huo shehena ya makasa zaidi ya 5000 yapo yakisubiri wateja.
Amewataka Bodi ya Korosho na wafanya bishara kutatua changamoto zilizoko upande wao ili mizigo ije kwa wingi kwani hali ilivyo sasa uwezo wa Bandari kuhudumia shehena ni mkubwa kuliko mizigo inayoingia.
Video ya tukio hii HAPA
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.