Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe: Gelasius Byakanwa ametoa miezi mitatu kwa wakazi wa Mkoa wa Mtwara kujiandikisha kwenye daftari la wakazi lililopo kila Mtaa.
Amesema kuwa kama muda huo utapita na mwananchi hajajiandikisha hatatoa adhabu yeyote, badala yake mwananchi atakosa huduma mbalimbali kutoka kwenye Ofisi za Serikali ikiwemo barua za utambulisho zinazotakiwa kwenye mabenki na huduma zingine.
Byakanwa amezungumza hayo leo wakati wa uzinduzi wa zoezi la Uandikishaji kwenye daftari la wakazi kwa Mkoa wa Mtwara lililofanyika kimkoa kwenye Viwanja vya Ofisi ya Kata Shangani Manispaa Mtwara-Mikindani. Aidha amewataka watendaji kutomkaribisha mgeni yeyote kwenye Mtaa kama hana taarifa za kujiandikisha kwenye mtaa alikotokea.
Amesitiza kuwa ili kuendelea kulinda amani, utulivu na kuondoa uhalifu kwenye maeneo yao ni lazima wananchi wakafahamiana kwa kujiandikisha kwenye daftari la wakazi lililoko chini ya Mtendaji wa Mtaa. Pia ameagiza mtu yeyote anapohamia kwenye mtaa ahakikishe amejiandikisha kwenye daftari hilo ili taarifa zake zingizwe.
Mkuu huyo wa Mkoa amezitaja faida zitokanazo na wananchi kujiandikisha kwenye daftari la wakazi kuwa ni pamoja na kusaidia Serikali kupanga bajeti, mahitaji, na huduma za jamii kwa watu wake kwa kuwa takwimu za idadi ya watu waliopo kwenye mitaa, kata, tarafa, wilaya, mkoa hadi Taifa zitakuwepo. Faida zingine ni pamoja na kuimarisha Ulinzi na Usalama.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa Mtwara-Mikindani Bi. Beatrice Dominic amesema kuwa Wananchi waliosajiliwa kwenye daftari la wakazi kwa Manispaa ni 46,704 Kati ya Wananchi 115,000 waliokadiriwa kwenye sensa ya watu na makazi ya 2012. Aidha amesema anatarajia baada ya uzinduzi huo wananchi watatimiza wajibu wao kwa kujiandikisha kwenye daftari hilo.
Ameongeza kuwa Daftari hilo litatunzwa na Mwenyekiti wa Mtaa husika na kwamba Mwenyekiti atapaswa kujaza fomu kila taarifa mpya zinapojitokeza zikiwemo vizazi, Vifo, kuhama na kuhamia. Aidha Mtendaji wa Mtaa atahakikisha daftari hilo linaingizwa Taarifa, linatunzwa na linatumika ipasavyo.
Daftari la wakazi lipo kisheria chini ya sheria ya Serikali za Mitaa Na. 6 ya mwaka 1982, na limechapishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI mwaka 2011.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.