Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Byakanwa amewataka wadau wa maaendeleo walioahidi kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika halmashauri ya wilaya ya Mtwara kukamilisha ahadi zao.
Hayo ameyasema leo Januari 30, 2019 wakati akipokea hundi ya shilingi milioni 13,258,042 kutoka kwa Meneja mahusiano Shirika la Mendeleo la Petroli Tanzania (TPDC), Marie Mselem kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa shirika.
Amesema TPDC waliahidi na leo wametekeleza ahadi. Ni vema na wengine nao wakakumbuka walichoahidi na kukamilisha.
“Baada ya kuzunguka halmashauri yote ya Wilaya ya Mtwara tuligundua shule kumi zilikuwa na matatizo ya vyumba vya madarasa. tuliitisha kikao cha wadau wa maendeleo. Baadhi wametimiza ahadi zao, wengine hawajatimiza. wako walioahidi fedha na wengine vifaa. Nawaomba wakamilishe kama walivyoahidi mbele ya wadau wenzao”. Amesema Byakanwa
Awali akiwasilisha hali ya ujenzi wa vyumba hivyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Omari Kipanga amesema katika harambee iliyofanywa na Mhe. Mkuu wa Mkoa mapema mwaka jana zilipatikana fedha na vifaa ambavyo thamani yake ilikuwa shilingi milioni 160. Mahitaji ya jumla zilitakiwa milioni mia sita kukamilsha miundombinu yote.
Milioni 160 zilizopatikana wakati huo zilitumika kunyanyua maboma 48 ambapo 16 kati yake yalikamilika kupauliwa na kuezekwa. Maboma 32 bado yanahitaji fedha ili yakamilishwe.
Amesema kwa upande wa Halmashauri wameshanunua Bando 159 za bati ambazo zinatosheleza kuezeka maboma yote 32. Hivyo bado wanahitaji nguvu ya ziada toka kwa wadau ili kukamilisha hatua nyingine za ujenzi.
Kwa upande wake Menja wa TPDC, Marie Mselem amewashukuru wananchi wa Mtwara kwa ushirikiano wao. Amesema Mtwara ni nyumbani hivyo Shirika linakumbuka kurudisha nyumbani kidogo wanachokipata.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.