Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenister Mhagama amesema Serikali itaendelea kuwasaidia wahanga wanaokutwa na majanga ya kibinadamu katika maeneo mbalimbali nchini huku akiitaka jamii nayo kushirikiana na Serikali kukabiliana na athari za matukio ya aina hiyo.
Waziri Jenister ametoa kauli hiyo wakati akishiriki katika zoezi la kugawa misaada yenye thamani ya Shilingi Milioni 231 kwa wahanga wa majanga ya kibinadamu katika vijiji vya Kitaya, Dindwa, Bandari na Michenjele katika Wilaya za Mtwara na Tandahimba na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni ishara ya Serikali inayojali Maisha ya wananchi wake.
Akiongoza zoezi la kugawa misaada ya mabati, magodoro, ndoo, mablanketi na mikeka kwa kaya 184 katika vijiji vya Kitaya, Dindwa na Bandari Wilayani Mtwara Mhe Mhagama amesema yanapotokea maafa katika eneo lolote, jamii inayozunguka inatakiwa kuwa ya kwanza kushiriki kuwafariji wahanga kwa namna yeyote badala ya kuisubiri Serikali.
“Ndugu zangu, sheria namba 6 ya mwaka 2022 ya usimamizi wa maafa inatutaka kufanya tathimini ya athari zilizopatikana baada ya tukio na baadae kutoa mkono wa pole kwa wahanga kama tunavyofanya na sio kulipa fidia” alisisitiza Waziri Mhagama.
Aidha akiwa katika Kijiji cha Michenjele Wilayani Tandahimba Mhe. Jenister Mhagama, amekabidhi misaada hiyo kwa kaya 160 za wahanga wa majanga mbalimbali ya kibinadamu na kuutaka uongozi wa Wilaya uliopewa dhamana ya kusimamia zoezi hilo kuhakikisha kila kaya inapata msaada kama ilivyoelekezwa.
“Ni matumaini yangu misaada hii mtaitumia kwa malengo yaliyokusudiwa , tumieni mabati haya kujenga nyumba zenu zilizoathirika, sitegemei kusikia mmeyauza, na nyinyi ninaowapa jukumu la kugawa sitegemei kusikia figisu figisu za aina yeyote katika zoezi hili” alionya Waziri Mhagama.
Pia Mheshimiwa Mhagama amelitumia zoezi hilo kuwahakikishia wananchi wa vijiji vyote vilivyopata msaada huo kuwa Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuwafikishia huduma zote muhimu katika maeneo yao huku akitolea mfano miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, vituo vya afya, maji , umeme, na barabara kama kielelezo cha jitihada za serikali kuboresha maisha ya wananchi wake.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed ameishukuru Serikali kwa kuthamini Maisha ya wanamtwara na kusema kuwa hiyo ni ishara tosha kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan inatanguliza mbele maslahi ya wananchi wake.
“Ndugu zangu, bila shaka nyinyi ni mashahidi kuwa mara zote tunapofikwa na majanga ya kibinadamu, Serikali inakuwa pamoja nasi, hivi karibuni ndugu zetu walipokumbwa na mafuriko katika kata za Mahurunga na pia katika baadhi ya Vijiji kule Newala haikutuacha nyuma” alisema Kanali Abbas.
Jumla ya msaada uliotolewa kwa kaya 346 katika vijiji 6 vya Wilaya za Mtwara na Tandahimba ni pamoja na mabati 5,700 , ndoo kubwa na ndogo 570 , blanketi 570 na mikeka 380 vyote vikigharimu kiasi cha shilingi Milioni 231.
Katika mgao wa vifaa hivyo Kila Kaya imepata mabati 30, ndoo za Maji kubwa 2 na ndogo 1, mablanketi 3, godoro 1 na mikeka 2.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.