Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mwanasheria Mkuu wa serikali Dkt. Adelardus Kilangi imetoa ufafanuzi kuhusu sakata la korosho lililotawala kwenye vyombo vya habari hivi majuzi. Sakata hilo liliwahusisha baadhi ya waheshimiwa wabunge ambao walionesha kutoridhishwa na pendekezo la serikali kufuta ushuru wa asilimia 65 wa fedha zinazotokana na mauzo ya korosho nje zilizokuwa zikielekezwa katika mfuko maalumu wa kuendeleza zao la korosho.
Akielezea Leo Bungeni kupitia video inayopatikana kwa Kubonyeza HAPA, Dkt. Kilangi anafafanua kuwa sheria mbalimbali za nchi hazizuii serikali kufanya uamuzi unaokusudiwa. Amezitaja sheria hizo kuwa ni pamoja na Cashew nut Board of Tanzania Act (1884), Cashew nut Marketing Regulations (1996), Maelekezo ya serikali ya mwaka 1998. Kesi iliyofunguliwa na Mfuko wa Kuendeleza zao la Korosho mwaka 1999, Waraka wa Baraza la Mawaziri Namba 42 wa mwaka 2005, Finance Act (2006), pamoja na ‘Memorandum of Understanding’ ya wadau wa korosho ya mwaka 2010.
Ameendelea kuwa hoja hiyo pia inaweza kupata ufafanuzi zaidi kupitia kesi ya Mfuko wa Kuendeleza zao la Korosho ya mwaka 1998 ambapo serikali ilishtakiwa baada ya kuzuia Bodi ya Korosho kupeleka fedha hizo kwenye mfuko wa kuendeleza zao la korosho. Kesi hiyo namba 2004 iliyofunguliwa mwaka 1999 ilipelekea mfuko kushindwa kesi mahakamani, kisha kushindwa tena baada ya kukata Rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa. Aidha Mahakama ilitoa ufafanuzi kuwa makusanyo hayo ni fedha za umma na kwamba bodi ya korosho inakusanya fedha hizo kwa niaba ya serikali na kwamba serikali ndiyo yenye maamuzi juu ya hizo fedha.
Pamoja na maamuzi ya mahakama ambayo yanaipa nguvu serikali bado utaratibu wa kuundwa kwa Mfuko wa kuendeleza zao la korosho haukuweka sheria ambayo inaizuia serikali kuondoa fedha hizo ambazo sasa inakusudia kuzielekeza hazina.
Anaeleza kuwa mwaka 2010 wadau walianzisha mfuko wa kuendeleza zao la korosho lakini bado Memorundum of Understanding iliyopelekea uamuzi wa kuunda Mfuko huo haikutaja iwapo export Levy itakuwa moja ya vyanzo vyao vya fedha. Aidha mfuko huo haukuanzishwa kwa sheria ya Bunge bali ulianzishwa kama Trust.
Mheshimiwa Mwenyekiti Serikali haiwezi kulipa fedha kwenye mfuko ambao haujaanzishwa kwa sheria iliyotungwa na Bunge’. Anaeleza Dkt Kilangi.
Sikiliza Vdeo HAPA
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.