Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mheshimiwa Evod Mmanda akipokea Vitabu toka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Elimu Tannzania Profesa Benadeta Kiliani
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mheshimiwa Evod Mmanda ameitaka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kuhakikisha inasimamia maudhui yanayozalishwa katika vitabu ili yalenge matakwa ya jamii ya watanzania. Amesema vitabu vinahifadhi maarifa ambayo ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa lolote duniani hivyo usimamizi imara wa maudhui yanayowekwa kwenye vitabu ni muhim kwa maendeleo ya Taifa.
Mheshimiwa Mmanda ameyasema hayo leo wakati akipokea vitabu vilivyotolewa na Tasisi hiyo kwa mkoa wa Mtwara katika hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Ufundi Mtwara.
Amesema hana mashaka na kazi ya Taasisi ya Elimu Tanzania kutokana na weledi wanaouonesha katika kusimamia kazi zao hivyo moyo huo unapaswa kuendelea ili kuzalisha taifa la wazalendo.
Akizungumzia juu ya mapokezi ya vitabu hivyo Mheshimiwa Mmanda ameshukuru serikali ya awamu ya tano kwa kuwa na nia ya dhati ya kulifikisha taifa katika malengo yaliyokusudiwa. Amesema serikali ya awamu ya tano tangu ilipoingia madarakani ililenga kuhakikisha kila mwanafunzi anakuwa na kitabu cha kujifunzia na azima hiyo imefikiwa
Ametoa wito kwa walimu wahakikishe wanavitumia vitabu hivyo badala ya kuvifungua ofisini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Elimu Tanzania, Profesa Benadeta Kiliani amesema zoezi la usambazji wa vitabu Tanzania Bara lilianza mwezi Februali mwaka huu na limekuwa likienda vizuri.
Amezitaka halmashauri zote zilizokwisha pokea vitabu hivyo wavisambaze haraka shuleni hatimaye kwa wanafunzi ambao ndio walengwa.
Amevitaja vitabu vinavyosambazwa kuwa ni vitabu vya kiada kuanzia darasa la kwanza hadi la Nne. Pia kiongozi cha Mwalim. Hadi Februali 27 mwaka huu walikuwa wamesambaza vitabu vya darasa la kwanza hadi la tatu kwa mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Tanga, Dodoma, Singida, Manyara Arusha na Mwanza. Aidha kati ya April 29 hadi Mei 5 mwaka huu watakuwa wameifikia mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Pwani na Mara.
Akizunguza kwa niaba ya Maafisa Elimu Mkoa wa Mtwara, Afisa Elimu Msingi, Halmashauri ya Mji wa Nanyamba, Said Farahani amesema uamuzi wa serikali kusambaza vitabu hivyo ni mzuri. Amesema hiyo ndiyo njia sahihi ya kulifikisha taifa katika maendeleo yaliyokusudiwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.