Mkoa wa Mtwara Umezindua rasmi mpango wa usafiri wa dharula wa akina mama wajawazito, wanaojifungua na watoto wachanga unaojulikana kama M-Mama ambao kitaifa ulizinduliwa mjini Dodoma Aprili 06 mwaka huu na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Katika uzinduzi huo uliofanyika katika Ukumbi wa Boma mjini Mtwara na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa afya, Mkuu wa Mkoa Kanali Ahmed Abbas Ahmed Kupitia hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Dunstan Kyobya aliyemwakilisha, amesema mkoa unakabiliwa na changamoto ya vifo vitokanavyo na uzazi na kusema kuwa anafarijika mpango huo umekuja wakati muafaka na utachangia kuleta mabadiliko.
Hotuba ya Kanali Abbas imeongeza kuwa pamoja na jitihada za wataalamu wa afya katika ngazi zote mkoani hapa, bado takwimu za vifo vitokanavyo na matatizo ya uzazi haziridhishi ambapo mwaka 2021 idadi ya vifo ilikuwa wakinamama 75 na mwaka huu wa 2022 mpaka kufikia siku ya uzinduzi wa mpango huo tayari wakinamama 79 walikuwa wamepoteza maisha.
“Ndugu washiriki wa kikao hiki Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuagiza kuhakikisha tunausimamia kikamilifu mpango huu ili kulinda afya ya mama wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua na pia afya ya mtoto, hivyo kwa pamoja sisi kama mkoa tumejiwekea mikakati itakayotuongoza kufikia lengo hilo” alisisitiza Kanali Abbas kupitia hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Dunstan Kyobya.
Aidha hotuba ya Kanali Abbas iliongeza kuwa ili kutekeleza agizo la Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa vitendo na kuhakikisha tatizo la vifo vya wakinamama na watoto linadhibitiwa, tayari Mkoa wa Mtwara umechukua hatua kwa kuboresha vitengo vya dharula za upasuaji vilivyokuwa vikipatikana katika vituo vya afya 24 pekee mpaka mwaka jana 2021 ambapo sasa vimeongezwa hadi 26 kufikia Disemba 2022.
Pia hotuba hiyo ya Mkuu wa Mkoa imezitaja jitihada nyingine zilizofanyika za kukabiliana na tatizo hilo kuwa ni pamoja na kuboresha na kupanua wigo wa upatikanaji wa vifaa tiba, dawa muhimu, damu salama pamoja na kuajiri wataalamu wapya na kuwajengea uwezo.
Kuhusu mpango wa usafiri wa dharura kwa akina mama wajawazito, wanaojifungua na watoto wachanga (M-Mama) Kanali Ahmed Abbas Kupitia hotuba yake iliyosomwa na Mhe Kyobya imebainisha mikakati ya mkoa wa Mtwara katika kuhakikisha mfumo huo unawanufaisha walengwa katika ngazi zote ikiwa ni pamoja na kuingia mikataba na wamiliki wa magari binafsi ili yaweze kutoa huduma wakati ambapo magari ya kubeba wagonjwa katika vituo husika yatakosekana.
“Bila Shaka kila mmoja wetu hapa anakubali mpango wa M-Mama ni mkombozi wa akina mama wajawazito na watoto wachanga, sote tunafahamu na tumeshuhudia katika maeneo yetu adha ya usafiri anayoipata mama mjamzito pindi anapopewa rufaa kutoka kituo kimoja kwenda kituo kingine chenye huduma ya kiwango cha juu, ukiangalia magari yaliyopo ni manane tu (08) na hayatoshelezi” alisisitiza kanali Abbas.
“Ninaamini kuanzia hivi sasa kupitia M-Mama tutawafikia wakinamama wajawazito wengi zaidi na kwa urahisi popote walipo ikiwemo katika vituo vya afya, zahanati na hata katika jamii yaani majumbani,bila shaka kwa kufanya hivyo ni matumaini yangu tunakwenda kuandika historia mpya katika suala zima la afya ya mama na mtoto mkoani kwetu” aliongeza Kanali Abbas katika hotuba yake iliyosomwa na Mhe Dunstan Kyobya.
Kuhusu ushiriki wa Halmashauri za Wilaya katika mpango huo, Kanali Ahmed Abbas Ahmed amewaagiza Wakurugenzi kusimamia kikamilifu mpango huu kwa kuteua waratibu wa usafiri wa dharula, kuteua wafanyakazi wa kuratibu dharula katika vituo vya afya, kutoa mwongozo wa kwa watendaji wa vijiji waweze kuwatambua wamiliki wa magari binafsi katika maeneo yao na pia watenge bajeti maalumu kwa ajili ya usafiri wa dharula.
Kwa upande wake Mratibu wa Uzazi Salama kutoka Wizara ya Afya Naibu Mkongwa amesema kuwa serikali imejiridhisha kuwa M-Mama itasaidia kuboresha Afya ya mama na mtoto na kwamba tafiti za hivi karibuni zimethibitisha kuwa Tanzania inamgawanyo mzuri wa idadi ya vituo vya afya na zahanati ambao kwa ujumla utarahisisha utekelezaji wa mpango huo.
Uzindunduzi wa M-Mama katika mkoa wa Mtwara unaufanya kuwa Mkoa wa 9 kati ya mikoa 14 nchini inayotarajiwa kunufaika na mpango huo ambao awali kati ya mwaka 2013 – 2021 ulifanyiwa majaribio katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza na kuonyesha mafanikio.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.