Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Halima Dendego akichangia damu katika moja ya matukio ya uchangiaji Damu Mkoani Mtwara
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Halima Dendego ameagiza Halmashauri ziweke mikakati imara kuhakikisha damu salama zinakusanywa. Amesema bila kuwa na utaratibu mzuri wa ukusanyaji wa damu vifo vya akina maam na watoto vitaendelea kuongezeka katika jamii. Dendego amesema hayo wiki hii wakati akifungua kikao cha Wadau wa Afya kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Uganga Masasi.
Amesema bila kutenga bajeti ya kutosha na kuwa na ushirikiano mzuri na watu wa Damu Salama, vifo vya akina mama wajawazito na watoto vitaendelea.
Sote tunafahamu kwamba upatikanaji wa damu salama maeneo yetu ya kutolea huduma ni jambo la msingi kwa sababu bila kuwa na damu salama tunaweza kupoteza uhai wa watu wengi, hivyo ni lazima tuhakikishe tunakuwa na Damu salama katika maeneo yetu. Pia tushirikiane na watu wa Damu Salama ili kurahisisha upatikanaji wa damu salama na kuhamasisha jamii katika halmashauri zetu kuchangia damu. Amesema Dendego.
Amesema mahitaji ya damu salama kwa mkoa wa Mtwara wenye Halmashauri 9 ni ‘unit’ elfu 12 kwa mwaka. Hivyo kunahitajika kuwepo na jitihada ya dhati ya kuhakikisha hospitali zote mkoani Mtwara zinakuwa na akiba ya kutosha.
Aidha, Mheshimiwa Dendego amewasifu Halmashauri ya Mji wa Masasi kwa kufikia lengo ambapo halmashauri hiyo kwa mwaka 2016 ilivuka lengo la ukusanyaji damu kwa asilimia 163.
Akizungumzia hali halisi ya ukusanyaji wa damu mkoani Mtwara Meneja wa Damu Salama kanda ya Kusini Pendaeli Sifueli amemsifu Mheshimiwa Dendego kwa kuwa mstari wa mbele katika kuchangia damu na kuhamasisha jamii katika suala la uchangiaji damu.
Amesema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 26 ya vifo vilivyokuwa vikitokea kabla ya kuanzihsa kwa matumizi ya Damu Salama vilikuwa vinatokana na upungufu wa damu. Sehemu kubwa ya waathirika walikuwa ni wajawazito na watoto.
Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kuchangia damu. Aidha katika kupambana na changamoto ya mabadilishano ya mahitaji ya damu salama sehemu mbalimblai hapa nchini upo mpango wa kufunga mfumo wa mawasilianio kwa maeneo yote nchini yanayotoa huduma ya Damu salama.
Amesema mfumo huo utamuwezesha mahitaji au ziada ya damu kutoka sehemu moja hadi nyingine kufahamika, kasha kubadilishana.
Kikao cha wadau wa afya kimeendelea kwa siku tangu tatu huku kikiwakutanisha wadau wote wa afya zikiwemo Taasisi za Umma na binafsi hapa mkoani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.