Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Kirumbe Ng’enda pamoja na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga Leo tarehe 09/09/2024 wamefanya ziara mkoani Mtwara kwa lengo la kukagua miradi inayotekelezwa na Wizara ya Nishati pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
“Pamoja na majukumu mengine, bunge pia lina kazi ya kuishauri na kuisimamia serikali; Leo tumekuja kuangalia na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Wizara kupitia TPDC ikiwa ni pamoja na gesi. Lakini pia kamati hii inaiagiza Tanesco wafanye matengenezo ya mitambo chakavu.” Alisema Mhe. Ng’enda.
“Hali ya Upatikanaji wa nishati ya umeme baada ya kusimikwa mtambo wenye kuzalisha umeme Megawat 20 unaozalishwa kwa gesi asilia imekuwa ya kuridhisha kwani wananchi na wawekezaji wanapata umeme wa uhakika.” Alieleza Bw. Patrick Kyaruzi, Mchumi kutoka Ofisi ya Mkoa wa Mtwara.
Aidha, Bw. Patrick aliongeza kueleza kuwa Mkoa wa Mtwara una vijiji 785 ambavyo katika mradi wa REA vijiji vyote vimeweza kuunganishwa Nishati ya umeme.
Miradi iliyotembelewa na kamati hiyo ni pamoja na visima vya uzalishaji gesi vya Mnazi Bay, miradi miwili ya kurudisha fadhila kwa jamii-CSR (Ujenzi wa kituo cha Polisi na Kituo cha Afya) inayotekelezwa na TPDC katika eneo la Msimbati pamoja na mitambo ya kuchakata gesi asilia iliyopo Madimba.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.