Viongozi wa Taasisi za Serikali watakiwa kutozuia utoaji wa taarifa.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mheshimiwa Evod Mmanda amewataka viongozi wa Taasisi za Serikali kutozuia taarifa muhimu kwa wananchi kuingizwa kwenye Tovuti.
Akifunga mafunzo ya siku saba ya uanzishaji wa Tovuti yaliyokuwa yakifanyika katika ukumbi wa Tiffany Diamond Hotel leo, amesema serikali ya Tanzania inasisitiza utawala bora na inaendeshwa kwa uwazi, hivyo suala la kubania taarifa halitavumilika. Amesema Lengo la serikali ni kuwafikia wananchi wote kwa Wakati na ndiyo maana imewaajili Maafisa Habari na TEHAMA ili kuhakikisha lengo hilo linafikiwa.
Mmanda ambaye aliambatana na Kaimu Katibu Tawala Mkoa Elias Nyabusani katika zoezi hilo amewataka Maafisa Habari wasisubiri wananchi waandamane hadi ngazi za juu kwa sababu ya kutopata taarifa sahihi bali wawe chanzo cha kuondoa usumbufu na wingu la upotoshaji wa taarifa kwa kuweka taarifa sahihi kwa Wakati kwenye tovuti.
Aidha mewataka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhakikisha wanasaidia kusukuma ajira za Maafisa TEHAMA na Maafisa Habari kwani ziko Halmashauri nyingi ambazo hazina wataalamu wa kada hiyo.
Kwa Upande wake Mkuu wa timu ya wawezeshaji, Edgar Mdemu amesema mradi huo unaodhaminiwa na USAID umezindukiwa leo kitaifa mjini Dodoma na kwamba wanatarajia matumizi ya Tovuti yatasaidia kurrahisisha shughuli za serikali na hivyo kusukuma maendeleo ya taifa.
Aidha, Afisa Habari wa Halmashauri ya Manispaaa ya Mtwara Mikindani, Jamad Omari ameshukuru kwa kupata mafunzo hayo na kwamba yamesaidia Manispaa ya Mtwara Mikindani kusukuma maendeleo hasa katika kipindi hiki ambacho wanaweka mazingira ya kuvutia wawekezaji.
Mafunzo ya utengenezaji wa Tovuti yalifunguliwa Machi 20 na kufungwa Machi 27 ambapo kitaifa zoezi la ufungaji limefanyika mjini Dodoma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.