Kaimu katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Bi Nanjiva Nzunda amewataka wadau wa sekta ya maziwa kuyatumia maadhimisho kitaifa ya siku ya unywaji wa maziwa shuleni kutoa elimu na kuwahamasisha wazazi na walezi kuwapa Watoto maziwa ili kuimarisha afya zao.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Bi Bahati Geuzye, kwenye kongamano la maendeleo ya tasnia ya Maziwa Katika Ukumbi wa Boma, Bi Nzunda amesema kuelekea maadhimisho ya kitaifa ya siku ya unywaji maziwa shuleni itakayofanyika Mkoani Mtwara Septemba 25 Mkoa utayatumia kama darasa kuwahamasisha wadau wake kufahamu umuhimu wa maziwa kwa Watoto shuleni.
“Sote tunafahamu sehemu kubwa ya familia katika jamii yetu zinakabiliana na changamoto ya kuwawezesha Watoto kupata mlo kamili kabla ya kwenda shule n ahata wanaporejea nyumbani baada ya masomo” Alisema Bi Nzunda.
Kaimu Katibu Tawala Nzunda aliongeza kuwa hali hiyo imekua ikichangia kupungua kwa umakini wa kujifunza miongoni mwa Watoto sambamba na kuathiri matokeo ya mitihani yao ya mwisho.Aidha Kaimu Katibu Tawala Bi Nzunda amewataka wazazi, walezi na walimu kuzingatia kanuni bora za utoaji lishe kwa Watoto shuleni ikiwa ni pamoja na kuhakikisha chakula wanachopewa kinajumuisha viini lishe vyote ikiwemo protini, wanga, mafuta, vitamini na madini muhimu.
“Ndugu zangu tumewasikia wataalamu wetu wakitueleza kuwa mtoto akipata glasi moja ya maziwa kwa siku atakuwa amepata lishe bora yenye virutubisho kwa afya yake, hivyo niwaagize walimu na wataalamu mliopo hapa nendeni mkalisimamie hili” aliongeza Bi Nzunda.
Pia Nzunda ameyataja mafanikio ya mpango wa maziwa shuleni kuwa ni pamoja na kuboresha ukuaji wa Watoto, kuongeza kiwango cha ufaulu, kuongeza kiwango cha maudhurio na kupunguza utoro na kujenga kizazi cha Watoto wenye afya bora.Maadhimisho hayo yanayofanyika Mkoani Mtwara yenye kauli mbiu “Mpe Mtoto Maziwa kwa maendeleo bora shuleni” yanalenga kuwakumbusha wazazi umuhimu wa lishe bora kwa Watoto shuleni sambamba na kuhamasisha matumizi ya maziwa ili kuimarisha afya zao.
Sept. 24, 2024
@bodi_ya_maziwa_tanzania @mifugonauvuvi @wizara_afyatz @ortamisemi
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.