Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed amewataka Waalimu na Viongozi wa Elimu waliohitimu mafunzo ya uongozi katika elimu kuitumia elimu waliyoipata kuongeza ufanisi katika sekta ya elimu mkoani humo.
Kanali Abbas ameyasema hayo katika hafla ya kuwatunukia vyeti wahitimu 1014 wa mafunzo hayo iliyofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari Mustapha Sabodo, na kusema kuwa anaamini ujuzi walioupata utachangia kuboresha utendaji kazi wao ikiwa ni pamoja kuwaongezea mbinu na umahiri wa kitaaluma ili kuusaidia mkoa kufikia malengo yake ya kupandisha kiwango cha ufaulu.
Katika mafunzo hayo yaliyotolewa na Wakala wa Maendeleo ya Elimu (Agency for Develepment of Education Management - ADEM) kwa muda wa wiki tatu yakiwashirikisha Wakuu wa Shule za Awali na Msingi, Sekondari na Maafisa Elimu kata, Kanali Abbas amewataka wahitimu wote kuwa mabalozi pindi watakaporejea katika maeneo yao ya kazi na kusisitiza kuwa anatarajia wataitekeleza kwa vitendo elimu hiyo na kuitumia kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
“Ndugu zangu viongozi leo ninafuraha kubwa ninapokabidhi vyeti hivi kwenu kwani katika matokeo ya Taifa ya mwaka huu 2022/2023 tumepiga hatua kubwa ikilinganishwa na mwaka jana, kwa dhati kabisa nawapongeza katika ngazi zote, Halmashauri, Wilaya na pia Mkoa kwa usimamizi mzuri uliowezesha matokeo haya kupatikana “ alisema Kanali Abbas.
Aidha, kanali Abbas amewataka waalimu waliohitimu mafunzo hayo kujenga mahusiano mazuri kati yao na wazazi ili waweze kuwahamasisha kutambua umuhimu wa kuwapeleka watoto wao shule ili kuongeza kiwango cha udahili mkoani Mtwara.
“Ukiangalia takwimu zinaonesha bado tupo kwenye asilimia 88.17 za uandikishaji, hizo ni takwimu za hivi karibuni nikimaanisha Februari 2023, naomba muongeze bidii kwa kuwahamasisha wazazi wengi zaidi wawaandikishe watoto wao katika shule za msingi na kwa wale waliofaulu kwenda sekondari wazazi wao wawajibike kuwasimamia” aliongeza kanali Abbas.
Pia Kanali Abbas, amewakumbusha waalimu na viongozi wa elimu kuhakikisha huduma ya chakula cha mchana kwa wanafunzi inapewa kipaumbele na kusisitiza kuwa utaratibu huo ndio silaha ya kuongeza ufanisi katika sekta ya elimu na pia kuwashawishi wanafunzi kupenda elimu.
Aidha Kanali Abbas ameipongeza ADEM, kwa kukubali kutoa mafunzo hayo na kusema kuwa Serikali ya Mkoa itahakikisha inawasimamia kwa karibu viongozi wote waliohitimu ili waweze kwenda sambamba na malengo ya mafunzo hayo.
Akiwasilisha taarifa ya mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Katibu Tawala Msaidizi Rasilimali watu Renatus Mongogwela amesema Mkoa kwa muda mrefu umekuwa na utamaduni wa kuwajengea uwezo viongozi na wataalamu wake kupitia kozi mbalimbali hatua ambayo imewaongezea weledi wa kutekeleza majukumu yao kikamilifu katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu.
Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wakuu wa shule za Msingi, Sekondari na Maafisa Elimu kata na kuwawezesha kusimamia ufundishaji na ujifunzaji fanisi wenye kuzingatia ujuzi kwa kutumia fursa na uwezo uliopo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.