Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Byakanwa akizungumza na walimu wa Shule za Msingi na Sekondari Wilayani Masasi katika vinjwa vya Ikulu Ndogo Masasi
Na; Joina Nzali
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Gasper Byakanwa amewataka walimu wa shule za msingi na sekondari wilayani Masasi kuwa na Mipango madhubuti itakayo pandisha ufaulu wa elimu. Hayo ameyasema leo katika kikao kazi na walimu wote wa Wilaya ya Masasi kilichofanyika katika viwanja vya Ikulu ndogo mjini Masasi.
Amesema mkoa wa Mtwara umekuwa ukishika nafasi za mwisho katika matokeo ya Mitihani ya Taifa ya darasa la Saba, kidato cha Pili na Nne kwa miaka mitatu mfululizo jambo ambalo walimu wanapaswa kujiuliza na kutoka mbinu bora ili kuhakikisha ufaulu unapanda.
“Mimi ninaamini walimu mkiamua kupandisha ufaulu mnaweza, siri kubwa ni kuweka mkakati wa pamoja wa namna ya kuhakikisha mitaala kwa madarasa ya mitihani yaani Darasa la Nne, la Saba, kidato cha Pili na cha Nne inamalizika mapema ili watoto waweze kupata muda wa kufanya mitihani ya kujipima yenye hadhi ya kitaifa kabla ya Mtihani wa Taifa” alisema Byakanwa.
Kuhusu changamoto ya mwamko mdogo wa elimu, Mkuu huyo wa Mkoa amewashauri walimu kuwa na vibao vilivyoorodhesha majina ya wanafunzi waliowahi kufanya vizuri katika ngazi mbalimbali kuanzia ngazi ya shule hadi taifa ili kuwapa ari ya ufaulu watoto wengine walioko shuleni.
Aidha Mheshimiwa Byakanwa ameelekeza kuwa shule itakayokuwa ya mwisho kiwilaya katika matokeo ya Mitihani ya Taifa ya mwaka 2018 viongozi wa shule hiyo watatoa maaelezo mbele ya mkuu wa mkoa kwa nini wameshika nafasi hiyo.
Mkoa wa Mtwara umekuwa haufanyi vizuri Mitihani ya Taifa ambapo katika matokeo ya kidato cha Nne mwaka 2017 Mkoa umeshika nafasi ya 22 Kati ya mikoa 26
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.