Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala leo Novemba 29,2024 amefanya ziara katika Kiwanda cha Kuzalisha Simenti cha Dangote kilichopo katika halmashauri ya Wilaya ya Mtwara vijijini ambapo amejionea miundombinu inayotumika katika uzalishaji wa bidhaa hiyo.
Mara baada ya kuwasili kiwandani hapo majira ya mchana Kanali Sawala alipewa taarifa ya mwenendo wa uzalishaji na Kisha akafanya ziara kukagua maeneo mbalimbali ikiwemo eneo linalotumika Kuzalisha malighafi, kituo cha kupokea gesi pamoja na mfumo mzima wa uzalishaji kuanzia Simenti inapotengenezwa mpaka kufikia hatua ya mauzo ambapo aliupongeza uongozi wa Kiwanda Kwa kusimamia vizuri uwekezaji huo.
Halikadhalika ziara hiyo ilimwezesha Kanali Sawala kukutana na madereva wanaosafirisha Simenti kutoka kiwandani hapo kuelekea maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi katika kikao kilichodumu Kwa takribani Saa 1:24 ambapo walipata fursa ya kuwasilisha hoja zao mbele yake.
Miongoni mwa hoja hizo ni pamoja na maslahi duni yasiyoendana uzito wa majukumu yao, kuchelewa Kwa mishahara pamoja urasimu wakati wa kutoa mzigo nje ya kiwanda ambapo wamekuwa wakipewa kauli zinazokinzana kuhusu kufunika mzigo.
Akitoa majibu baada ya kusikiliza pande zote, Kanali Sawala amesema serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki Ili kuhakikisha wawekezaji pamoja na jamii inayozunguka eneo la mradi inanufaika.
"Ndugu zangu madereva bila shaka Kila mmoja wenu ni shuhuda wa faida tunayoipata kupitia Kiwanda hiki ikiwemo ajira, hivyo nawasihi wapeni ushirikiano wa kutosha wawekezaji hawa, jengeni utamaduni wa kutatua changamoto zenu Kwa njia ya Maridhiano sio manung'uniko au migomo" alisema Kanali Sawala.
Kuhusu hoja ya kuchelewa Kwa mishahara ya madereva, Kanali Sawala ameuagiza uongozi wa Kiwanda hicho kuweka utaratibu rafiki utakaohakikisha Kila dereva anapata mshahara wake Kwa wakati ifikapo mwisho wa mwezi.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa aliambatana na kamati za usalama za Mkoa na Wilaya, watendaji na viongozi kutoka taasisi za umma pamoja na wataalamu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.