Kuelekea miaka 19 bila Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere wakazi wa Mtwara Mikindani wameiomba serikali kukarabati nyumba aliyofikia mwalimu Nyerere wakati wa harakati za mapambano ya uhuru. Nyumba hiyo iliyojengwa na Mahajub Mahamoud mmoja wa wanajeshi wa jeshi la Mkoloni imekuwa gofu na kuta zake zimeanza kudondoka.
Akizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii wakati wa uzinduzi wa Mji Mkongwe wa Mikindani mapema mwezi huu Mzee Mohamed Kidume ambaye ni moja ya wazee maarufu mjini Mikindani amesema kwa wakati huo nyumba hiyo iliyoko ndani ya hifadhi ya mji Mkongwe wa Mikindani ndiyo nyumba iliyoonekana kuwa na hadhi ya kulala mgeni maarufu kama mpigania uhuru wa Tanganyika mwalimu Julius kambarage Nyerere. Pamoja na umaarufu huo nyumba hiyo imetekelezwa na sasa inaelekea kuanguka.
“Jambo ninalosikitika ni kwamba chama hakitaki kutengeneza hii nyumba, na serikali haitaki kusaidia vilevile. Leo umekuja umekuta zile kuta. Atakapokuja mtu mwingine atakuta huo ukuta haupo. Tafadhali nyumba inakufa na tutakuwa hatuna faida yoyote. Amesema Mzee Kidume”.
kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Japhet Hasunga amepokea ushauri huo na kumuagiza katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Aloyce Nzuki kuhakikisha nyumba hiyo inakarabatiwa na kukamilika ndani ya mwaka mmoja.
“…na nyinyi kama Wizara ile ya Mwalimu muisimamie. Nawapa mwaka mmoja mhakikishe mmeikarabati yote na imekamilika”.
Akilezea historia ya ujenzi wa Nyumba hiyo Mzee Kidume amesema ilijengwa na Mtanzania aliyejulikana kwa jina la Mahamoud ambaye alikuwa askari wa jeshi la mkoloni makazi yake yakiwa Dar es Salaam.
Aidha ujenzi huo ulikuwa ukisimamiwa na kaka yake aliyejulika kwa jina la Ahmed Adam wakati huo Mahamoud akituma fedha kutokea Ujerumani alikokuwa vitani.
Hata hivyo Mahamoud hakuweza kuiona nyumba hiyo kwani alifariki akiwa vitani.
Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Medard Kalemani amewaka watanzania kuchangumkia fursa iliyotolewa na serikali ya kuuunganishiwa umeme kwa kutumia kifaa kinachojulikana kama Umeme Tayari (UMETA). Amesema kifaa hicho kinamuepusha mtumiaji na gharama za kufanya wiring na hivyo kupunguza gharama za kuingiza umeme kwenye nyumba.
Waziri ameyasema hayo jana katika maeneo tofauti alipokuwa katika ziara yake ya siku mbili mkoani Mtwara.
“Serikali imeamua kuwapungumzia gharama wananchi kwani ukishaweka hicho chombo hulazimiki tena kufanya ‘wiring’ kwa nyumba za wastani, hasa nyumba zenye chumba kimoja hadi vinne. Kwa vile hicho kifaa kinafaa kwa matumizi yote isipokuwa viwanda tunawashauri wnanchi wavitumie. Pia tunashauri vifaa hivi vitumike kwenye taasisi za Umma kama ofisi za vijiji vituo vya afya, vituo vya polisi, zahanati na maeneo mengine ambayo kimsingi si lazima sana ufanye wiring.”
Amesisitiza kwamba serikali imewataka wakandarasi wahakikishe wanavitoa kwa wateja wa kwanza mia moja hadi mia mbili hamsini. baada ya hapo vinakuwa vinauzwa kwa bei ya serikali ambayo ni shilingi 36,000.
Pamoja na punguza hilo amesema serikali bado inaendelea na punguza la kuingiza umeme kupitia mradi wa REA ambapo gharama yake ni shilingi elfu 27 tu.
Waziri wa Fedha na Mipango Dr. Philip Mpango ameahidi kutatua changamoto ya usafiri kwa kituo cha Forodha Kilambo kilichoko wilayani Mtwara katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji.
Kituo hiki kimekuwa kikifanya kazi katika mazingira magumu kutokana na tatizo la gari la usafiri kwa wafanyakazi hali ambayo imekuwa ikisababisha usumbufu katika suala la ulinzi na ukusanyaji wa mapato.
“Kituo chetu cha forodha hakina gari na mpaka wetu ndio hivi uko wazi kabisa, wananchi wanatembea, wanakatiza hapa mtoni, kwa hiyo udhibiti kiusalama, kimapato unakuwa mgumu sana. Tumekubaliana na viongozi wa mamlaka ya mapato kwamba kabla ya tarehe 15 mwezi wa tisa wawe wameleta gari kwa ajili ya kuhudumia kituo hiki”.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalma Wilaya ya Mtwara ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mheshimiwa Evod Mmanda amemshukuru Mheshimiwa Waziri. Amesema muingiliano wa watu wa Mtwara na Msumbiji ni mkubwa kwa sababu ni watu wa jamii moja, kabila moja na dini moja. Amesema kwa hali kama hiyo ni rahisi mtu mwenye nia mbaya kujipenyeza. Hata hivyo bado ulinzi wa mpaka umeimarika.
“Hatujawa na tatizo na ndio maana tunajivuna kwamba Mtwara iko shwari. Tunazungumza kwa kifua mbele kwamba wenye kuja waje. Mtwara iko salama Mtwara ni mahali pazuri panakalika.” Amesema Mmanda.
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.