Tume huru ya taifa ya Uchaguzi imetangaza kuwa tarehe 28 Januari hadi 03 Februari 2025 zoezi la Uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura litaanza katika Mkoa wa Mtwara kwa awamu ya kwanza.
Akizungumza wakati wa mkutano wa tume na wadau wa uchaguzi uliofanyika mapema leo tarehe 16 Januari 2025, Mwenyekiti wa Tume hiyo Mhe. Jaji (R) Jacobs Mwambegele alieleza kuwa Tume katika kuhakikisha kwamba inaenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ikiwa ni pamoja na kurahisisha zoezi la uboreshaji wa Daftari, imeboresha mfumo wa uandikishaji ambao kwa mara ya kwanza utamuwezesha mpiga kura aliyepo kwenye Daftari kuanzisha mchakato wa kuboresha taarifa zake au kuhama kituo kwa kutumia aina yoyote ya simu ya kiganjani au kompyuta.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tume huru ya taifa ya Uchaguzi, Ndg. Ramadhan Kailima alieleza kuwa zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura litahusu kuandikisha wapiga kura wapya, kutoa kadi mpya kwa waliopoteza au kadi kuharibika, kurekebisha taarifa mfano majina, kuhamisha taarifa kwa waliohama maeneo pamoja na kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuukana uraia wa Tanzania na kifo.
“Wale wenye kadi za mpiga kura zilizotolewa mwaka 2015 na 2020 iwapo hawana taarifa iliyobadilika basi uboreshaji huu hauwahusu. Lakini kwa wale waliopata kadi kabla ya mwaka 2015 hata kama hakuna taarifa iliyobadikika, watalazimika kujiandikisha upya kwenye daftari la wapiga kura.” Alieleza Ndg. Kailima
Katika hatua nyingine, Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi imeweka wazi kuwa Wafungwa wa magereza waliohukumiwa kifungo cha chini ya miezi sita na mahabusu kwa mujibu wa kanuni ya 15(2)(c) ya Kanuni za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura za mwaka 2024 wana haki ya kuandikishwa kuwa wapiga kura.
Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga kura ni kwaajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 kuwachagua Madiwani, Wabunge na Rais. “Kujiandikisha kuwa mpiga kura ni msingi wa uchaguzi bora.”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.