Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala ametoa rai kwa viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mikindani kushirikiana katika kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuwafuatilia mafundi kwa ukaribu ili kuhakikisha miradi inatekelezeka kwa viwango vizuri.
Kanali Sawala ametoa rai hiyo mapema leo tarehe 23 Desemba 2024 alipokuwa akitembelea miradi ya maendeleo.
“Injinia, Mkuu wa Wilaya pamoja na viongozi wengine wote, niwaombe msimamie kwa ukaribu shughuli za ujenzi ili kuepuka gharama za ziada zitakazoweza kujitokeza ikiwa fundi amefanya kosa litakalogharimu kuvunja na kujenga tena.” Alieleza Kanali Sawala
Miradi iliyotembelewa na Mkuu wa Mkoa ni pamoja na ujenzi wa jengo la ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) ambao unakadiriwa kugharimu shilingi Bilioni 1.6 mpaka utakapokamilika Machi 2025. Ujenzi wa madarasa mawili na matundu sita ya vyoo katika shule ya msingi Magomeni.
Aidha, Kanali Sawala amekagua mradi wa maboresho ya Miundombinu ya usambazaji maji mijini Mtwara wenye jumla ya gharama ya Shilingi Bilioni 29.29 utakaojumuisha ujenzi wa matenki manne makubwa yenye uwezo wa kusambaza maji hadi lita laki sita kwa siku na uchimbaji wa visima viwili vikibwa.
Mradi mwingine uliotembelewa na Mkuu wa Mkoa ni wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani katika eneo la Mradi wa Samia City Mtaa wa Mjimwema ambao tayari umepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 3 kwa awamu tatu tofauti.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.