Tamasha kubwa la Msangamkuu linalofanyika kila mwisho wa mwaka katika fukwe za Msangamkuu, halmashauri ya wiłaya ya Mtwara zimeanza rasmi zikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe.Abdallah Mwaipaya.
DC Mwapaya ameongoza shamrashamra hizo leo tarehe 28 Desemba 2024 akishiriki katika matembezi (Jogging) yaliyohusisha vikundi na watu mbalimbali kutoka Mtwara na maeneo ya jirani.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, Mkuu huyo wa Wilaya amewasisitiza wananchi kutoka Mtwara na maeneo mengine nchini kuendelea kutembelea fukwe za Msangamkuu kwa ajili ya burudani mbalimbali na kupumzika katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.
“Hili ni tamasha kubwa ambalo linalenga kuutangaza mkoa wetu pamoja na vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo hususan utalii wa fukwe, niwakaribishe wananchi wote wanaoishi Mtwara na wageni mbalimbali waliikuja Mtwara wafike na kushuhudia mambo mbalimbali” amesema Mhe. Mwaipaya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa tamasha la Msangamkuu 2024 ambalo inafanyika kwa mara ya nne Ndugu Othmani Kambi, amesema tamasha hilo limeendelea kukua na lengo ni kulifanya kuwa kubwa na la kimataifa.
“Tunatarajia kuliona tamasha hilo likiwa kubwa zaidi, ukiangalia lilipoanza na hapa lilipo kuna mabadiliko makubwa kutokana na maboresho yaliyofanyika, tuna siku tano hapa za kufurahia mambo mbalimbali na tutahitimisha Disemba 31 kwa Mkesha Mkubwa wa kuupokea mwaka 2025” amesema Kambi
Naye Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Bi. Nanjiva Nzunda amewahakikishia wananchi wote watakaofika Msanga Mkuu kuwa Serikali imeweka mazingira ya wao kufurahia kwa kupata huduma zote muhimu za kijamii.
Amesema Tamsaha la mwaka huu limekuwa na maboresho makubwa zaidi na wananchi watakaofika watajionea utofauti huo hivyo kuwasisitiza kufika kwa wingi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.