Miongoni mwa fedha zinazokadiriwa kukusanywa kwa mwaka 2025/26 kiasi cha Shilingi Bilioni 29.61 kutoka mapato yasiyolindwa, Halmashauri za mkoa wa Mtwara inatarajia kutumia zaidi ya Shilingi Bilioni 11 kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo Shilingi Bilioni 2.96 zitatumika kwaajili ya mikopo ya 10% kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Bw. Abdilah L. Mfinanga, Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu akiwasilisha taarifa ya mapitio bajeti ya nusu mwaka wa fedha 2024/25 na makadirio ya mipango ya bajeti kwa mwaka fedha 2025/26 katika kikao maalum cha Kamati ya Ushauri ya mkoa (RCC) kilichoongozwa na Mhe. Kanali Patrick Sawala ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara mapema leo tarehe 07 Machi 2025 alieleza kuwa mkoa wa Mtwara unatarajia kukusanya na kutumia Shilingi Bilioni 290.29.
“Niwapongeze Wakurugenzi wa Halmashauri zote na watumishi kwa ufuatiliaji mzuri kuhakikisha mapato yanakusanywa. Mpaka mwezi Februari 2025 makusanyo yamefikia 108% ni matumaini yangu mpaka tukimaliza mwaka wa fedha mwezi Juni tutazidi kufanya vizuri.” Alieleza Kanali Sawala
Katika hatua nyingine Kanali Sawala amezitaka kila Halmashauri zitenge fedha za ununuzi wa madawati, viti, meza na vifaa tiba huku akisisitiza matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mpango na bajeti ya mwaka 2025/26, umeandaliwa kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti Na.11 ya mwaka 2015 ambapo Wizara, Mikoa, Halmashauri na Taasisi nyingine za Serikali zinapaswa kuandaa mipango na bajeti ili ipitishwe na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.