Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mtwara Yusufu Nanilla amemtaka Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya korosho Nchini Francis Alfred kutatua changamoto iliyosababisha kushuka uzalishaji wa zao la korosho. Amesema katika miaka ya 1990 uzalishaji wa korosho Mkoani Mtwara ulikuwa mkubwa ukilinganisha na miaka ya hivi karibuni.
Kauli hiyo ameitoa leo katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya mkoa wa Mtwara kilichofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu Tawi la Mtwara. Amesema korosho ni zao muhimu na ndiyo maana mikoa mingi imejitokeza kuanza kulima na kwamba kama mkoa wa Mtwara utaendelea kulalamika na kuibua sababu zisizo na msingi, zao hilo litaendelea kushuka.
Awali akiwasilisha taarifa ya zao hilo Mkurugenzi wa Bodi hiyo Francis Alfred alisema uzalishaji wa korosho umeshuka musimu wa 2019/2020 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa magunia ya kufungashia pamoja na mabadiliko ya Tabia Nchi. Msimu wa mwaka 2019/2020 mkoa ulizalisha tani 132,553 tofauti na uzalishaji wa mwaka 2018/2019 ambapo mkoa ulizalisha tani 124,041.58. hata hivyo ongezeko hilo linakinzana na uzalishaji mkubwa uliokuwa ukifanyika kwa misimu ya mwaka 2017/2018 kurudi nyuma jambo ambalo linamfanya mwenyekiti wa Ccm mkoani Mtwara bwana Nanilla kuhoji ni kwa nini uzalishaji umeshuka hivyo.
Amesema changamoto ya vifungashio inaweza kuwa moja katika changamototo nyingi ambazo zikifanyiwa kazi uzalishaji utapanda.
“Wako wataalamu wengi humu ambao walishiriki kupandisha uzalishaji katika miaka ya 90, ambapo uzalishaji ulikuwa unafikia zaidi ya tani 190,000. Watumieni hao, mtowe elimu kwa jamii. Hadhi ya zao la korosho itarudi kama kawaida.”
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa ameunga mkono hoja hiyo na kuitaka Bodi ya Korosho kuitisha kikao ili kujadili sababu mbalimbali zinazogusa zao la korosho ikiwemo kutokupanda kwa bei wakati mahitaji ya wanunuzi yalikuwa makubwa. Amesema takwimu za uzalishaji msimu wa 2019/2020 mahitaji ya wanunuzi ilikuwa ni tani 496,667 ikilinganishwa na kiasi kilichozalishwa cha tani 132,553. Aidha, korosho hiyo iliuzwa kati ya shilingi 1400 na 2890.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.