Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, CPA. Bahati Geuzye ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali kuanzisha miradi itayoweza kuwaingizia mapato na kupunguza utegemezi kwa wafadhili kwani sera za wafadhili zinapobadilika inaweza kuathiri utekelezaji wa miradi husika.
CPA. Geuzye ametoa rai hiyo leo tarehe 28 Juni 2025 alipokuwa akifungua Jukwaaa la mashirika yasiyo ya kiserikali lililolenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa miradi na afua mbalimbali mkoani Mtwara kwa kipindi cha mwaka 2020/21-2024/25.
Mkoa wa Mtwara ni miongoni mwa mikoa ya Tanzania inayotekeleza miradi mbalimbali kwa kupitia Mashirika yasiyo ya Kiserikali ukiwa na Mashirika 77 yaliyo hai.
“Niwaombe muendelee kushirikiana na watendaji wa Serikali, wakiwaelekeza kufuata kanuni na utaratibu ni vema mkafanya hivyo. Pia mnapoweka mipango yenu ya utekelezaji kwa jicho la pekee niwaombe muweke vipaumbele maeneo ya pembezoni ili walengwa wote waweze kufikiwa.” Alieleza CPA. Geuzye
Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Bw. Abdillah Mfinanga ameeleza mafanikio yaliyofikiwa na mashirika hayo ni utekelezaji wa miradi 96 iliyowanufaisha jumla ya watu 759,920.
Makundi yaliyonufaika na miradi hiyo ni pamoja na Vijana, Wakina Mama, Wazee, Watoto, watu wenye ulemavu, Wasichana, wanafunzi Katika Vyuo, shule za Msingi na Sekondari, Wafungwa na warahibu wa madawa ya kulevya, wagonjwa wa hospitalini na wa Majumbani, Watendaji wa Kimila kwa Maana ya Mangariba na Makungwi, Wataalamu wakuu wa Vitengo na Idara za Serikali, Wakulima na Wafugaji pia na Vijana wa Sekta ndogo ya usafirishaji (Boda boda).
Kauli mbiu ya Jukwaa hilo mwaka huu inasema, “Tathmini ya mchango wa NGOs katika maendeleo ya Taifa 2020/21-2024/25 mafanikio, changamoto, fursa na matarajio.”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.