Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Mhe. Abdallah Mwaipaya kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Mtwara mapema leo tarehe 14 Agosti 2025 ametoa rai kwa viongozi wa vijiji vilivyonufaika na mradi wa kilimo cha bustani uliofadhiliwa na Ubalozi wa Japan nchini Tanzania kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo (UNDP) kuweka utaratibu wa kulinda miundombinu ili isiharibiwe na wenye nia ovu ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua kwa watakaobainika.
Katibu wa kwanza wa Ubalozi wa Japan nchini Tanzania, Bw. Jin Hashimoto ameeleza lengo la mradi huo ni kujenga ustahimilivu na msingi wa kibiashara kwa wakulima hususan walioathirika na mvua pamoja na uelewa kwa viongozi wa mkoa juu ya namna ya kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Nae, mwakilishi mkazi wa UNDP, Bw. John Rutere ameipongeza ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kwa kuwezesha kufanikisha mradi kwa kuwafikia wakulima. Pia ametoa rai kwa serikali ya mkoa kuendelea kuchukua tahadhari za changamoto zinazoweza kuwakabili wakulima.
Mkurugenzi wa Ushirika wa Wajasiriamali Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUGECO), Bw. Revocatus Kimaro ameeleza kuwa mradi huo uwezesha wakulima kujifunza teknolojia mpya ikiwa ni pamoja na kuongeza soko la mazao ya bustani kwani sasa mazao ya wakulima hao yanauzwa nchi ya Comoro.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Newala, Mhe. Alhaji Rajabu Kundya apongeza mradi huo kwani ni fursa inayowawezesha wakulima mkoani Mtwara kuwa na kipato cha mara kwa mara kutokana na mazao ya bustani badala ya kusubiri mazao ya msimu kama korosho, ufuta na mbaazi.
Mradi huo wa kuongeza urejesho jumuishi na kujenga ustahimilivu kwa jamii zilizoathirika na mafuriko na kilimo cha bustani Mtwara ulianza kutekelezwa mwaka 2024.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.