Mwenyekiti wa Kamati ya michezo mkoa wa Mtwara ambae pia ni Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara CPA. Bahati Geuzye amewapongeza walimu, walezi na wanafunzi wa shule za Msingi mkoani Mtwara kwa maandalizi mazuri ya mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Tanzania kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) yanayotarajiwa kuanza tarehe 07 Juni 2025 mkoani Iringa.
CPA. Bahati ametoa pongezi hizo leo tarehe 03 Juni 2025 alipotembelea kambi ya mazoezi ya wanafunzi hao ambapo jumla ya wanafunzi 120, walimu wa michezo 16 pamoja na daktari mmoja wanatarajia kusafiri siku ya kesho.
“Sisi kama Mkoa tunaahidi kuangalia ustawi wenu mnapokuwa katika kambi, mnaposafiri na mtakapofika kule. Mimi sina shaka kuwa mtarudi na vikombe tena vingi kabisa.” Alieleza CPA. Bahati.
Aidha, CPA. Bahati amewashukuru wazazi na walezi wa watoto wanaoshiriki mashindano hayo kwa kwakuwaruhusu watoto wao waweze kushiriki huku akiwasisitiza watoto hao kufanya michezo pamoja na kuzingatia vema masomo yao.
Michezo itakayochezwa katika mashindano hayo ni pamoja na mpira wa miguu, mpura wa mikono, mpira wa wavu, soka maalumu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, mpira wa mikono, mpira wa kengele kwa wasioona na wenye uoni hafifu, mpira wa kikapu, riadha, kwaya, ngoma pamoja muziki wa kizazi kipya.
Mashindano ya UMITASHUMTA 2025 yamebebwa na Kauli mbiu isemayo “Viongozi bora ni msingi maendeleo ya Taaluma, Sanaa na Michezo; Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025 Kwa Amani na utulivu.”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.