Waziri wa Nishati Mhe. Medard Kalemani amezindua matumizi ya Gesi Asilia majumbani kwa mkoa wa Mtwara. Mradi huu wa awali kwa mkoa wa Mtwara utagharim shilingi Bilioni 3.7 ambazo ni fedha za ndani za Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Akizindua mradi huo Mhe. Kalemani amesema Awamu ya kwanza ya mradi itazihusisha kata tatu za Reli, Shangani na Likombe zilizoko Manispaa ya Mtwara Mikindani ambapo jumla ya wateja mia tatu watafikiwa. Amesisitiza kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali zao huku ikipunguza uharibifu wa mazingira.
Amesema asilimia 71.25 ya watanzania wanatumia mkaa na kuni ambazo zinapelekea uharibifu wa mazingira.
Kuhusu matumizi ya gesi asilia kwenye magari amesema wako katika mazungumzo na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA-Mtwara) kwa lengo la kupata eneo ka kusimika miundombinu ya utoaji wa huduma hiyo. Lengo ni kukamilisha mradi huo ifikapo Desemba mwaka huu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Evod Mmanda ameipongeza serikali kwa kuwezesha utekelezaji wa mradi huo. Amesema mkoa wa Mtwara ni moja ya maeneo ambayo yameathirika na ukataji wa miti kwa ajili matumizi ya kuni na Mkaa.
“Kwa asili wilaya na mkoa wetu si eneo lenye miti mikubwa. Ni eneo lenye miti midogo na vichaka kiasi. Ukatataji wa miti kwa ajili ya uchomaji wa Mkaa ulikuwa ukitupeleka kwenye hatari kubwa, Ujio wa Gesi asilia utasaidia kwa kiasi kikubwa kurudisha mazingira katika hali yake.” Amesema Mmanda.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania(TPDC), James Mataragio amewaondoa mashaka wananchi na watumiaji wa gesi asilia kwamba iko salama sana tofauti na gesi ya mitungi.
“Gesi hii ni salama na zaidi ukilinganisha na gesi ya kitungi (LPG) ama mafuta ya taa au kuni. usalama huu unasabaishwa na tabia yake kwani ni nyepesi kuliko hewa tunayovuta hivyo kupelekea kupotea hewani mapema ikitokea imevuja kwenye jiko kwa namna yoyote na kuondoa uwezekano wa kulipuka na kusababisha moto.”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.