Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa ameagiza kiwanda cha Ushirikika cha Chakama kilichouzwa kwa shilingi milioni 40 kiwe chini ya ofisi mkuu wa wilaya ya Masasi wakati taratibu za kukiendesha kwa maslahi ya wanachama husika zikiandaliwa.
Kabla ya kiwanda hicho kuuzwa kwa njia ya mnada kwa gharama ya milioni 40 kilifanyiwa tahmini na kubainika kuwa thamani yake ilikuwa ni takribani milioni 656.
Akiwasilisha maamuzi yaliyotokana na kamati aliyoiunda mapema mwaka huu Byakanwa amesema kiwanda hicho kilitokana na umoja wa wakulima, wazalishaji na wabanguaji wa korosho kutoka vijiji vya Chakama, Mpindimbi, Maugura, Chiungutwa, Mwena na Temeke huko Masasi ambao waliunda kampuni ya Masasi High Quality Farnmers product (MHQP).
Byakanwa amesema sakata la kuuzwa kwa kiwanda hiki lilitokana na mahitaji ya mkopo wa shilingi milioni 5 kwa ajili ya kumlipa mkaguzi wa hesabu za kampuni. Taarifa ya mkaguzi huyo ilihitajika kwa ajili ya kupata ufadhili wa shilingi bilioni 1.6 kutoka kwa Shared Interest yenye makao yake Nairobi Kenya.
“Baada ya kusaini mkataba mkopeshaji alitaka mkataba upitiwe tena na mwanasheria (wakili). Wakili akashauri kila upande wa mkataba uongeze dhamana ya mali isiyohamishika. Bodi ya kampuni ikaweka dhamana ya kiwanda kinachokadiriwa kuwa na thamani ya shilingi milioni 656 bila kuitisha mkutano mkuu wa wanachama. Mkopeshaji akaweka dhamania ya nyumba yake yenye thamani ya shilingi milioni mia moja” amesema Byakanwa.
Byakanwa anaendeela kuwa baada ya kushindwa kulipa deni hilo mkopeshaji bwana Abdul Mohamed Satma alifungua kesi na kushinda mahakamani jambo ambalo lilipelekea kampuni kukata rufaa Mahakama Kuu kanda ya Mtwara.
“Kampuni iliamua kukata rufaa na kumlipa wakili Davis Aloycee Misingo milioni nne kwa ajili ya kazi hiyo...baada ya hapo si viongozi wa kampuni wala wakili wao aliyehudhuria mahakamani na hivyo kupelekea mahakama kufuta kesi”.
Kampuni ya Udalali ya D&G Auction and CO, LTD ilitangaza mnada wa kuuzwa kiwanda hicho ambapo Mzee Saidi Khatau aliibuka mshindi na kukinunua kiwanda hicho kwa shilingi milioni 40.
Pamoja na kasoro nyingi za taratibu za ukopaji hadi mnada kamati ilibaini kuwa katika mgawanyo wa fedha hizo ambazo Mdai ambaye ni Bwana Abdul Mohamed alilipwa shilingi 25,075,000, zilizobaki zote zilichukuliwa na kampuni ya udalali.
“Swali ninalojiuliza, kama kiwanda kingeuzwa kwa shilingi milioni mia moja au mia tatu, kampuni ya udalali ingelipwa shilingi ngapi? Au kama mnunuzi angekosekana, dalali asingepata ujira wake? Angeupata kwa nani?,”alihoji Byakanwa.
Byakanwa anaendelea kubainisha maswali ambayo yanazua utata wa mchakato wote kuwa hapakuwa na uwiano wa thamani ya kiwanda na pesa inayodaiwa.
“Siyo mahakama iliyojiridhsisha na thamani ya kiwanda wala taratibu za mnada kwani hata thamani ya kiwanda kulingana na mthamni wa serikali ni shilingi 270,000,000 bila kuweka gharama za mashine na mitambo mingine,”
Hata hivyo anasema malipo ya kampuni yalipwaswa kulipwa na kampuni ya MHQFP na siyo kampuni kujilipa kutokana na pesa ya mnada.
Kasoro nyingine zilizogundulika na kamati ni kutofuata taratibu za malipo kwani mshindi alipaswa kulipa asilimia 25 siku ya mnada lakini hakufanya hivyo na badala yake alilipa siku nne baadaye kinyume na kipengele cha nane cha amri/Tangazo la mnada.
Aidha malipo ya asilimia 75 mbayo yalipaswa kulipwa ndani ya siku thelathini tokea siku ya mnada vilevile pesa za malilipo zililipwa kwa Abdul Mohamed Satma (mdai) badala ya kulipwa kwa dalali.
Pamoja na uamuzi wa kukiweka kiwanda mikononi mwa serikali, Mheshimiwa Byakanwa ameagiza vyombo vya ulinzi na Usalama vikiongozwa na TAKUKURU kuwakamata na kuwahoji viongozi wengine wote waliohusika katika mchakato huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.